LONDON, Uingereza
KWA miaka mingi, El Classico imejijengea umaarufu mkubwa si tu kwa sababu ni mechi inayokutanisha miamba ya soka la Hispania, Barcelona na Real Madrid, bali pia ni dakika 90 zinazohusisha wachezaji wa daraja la juu katika ulimwengu wa soka.
Baadhi ya mastaa waliowahi kucheza El Classico kwa nyakati tofauti ni David Beckham na Zinedine Zidane na kwa miaka ya hivi karibuni ni Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Neymar na Luis Suarez.
Kwa sasa, El Classico ni shoo ya Lamine Yamal na Raphinha kwa upande wa Barcelona, huku Madrid ikiwa na Kylian Mbappe, Jude Bellingham na Vinicius Jr.
El Classico au ‘The Classic’ kwa Kiingereza, ilianza mwaka 1902 na kabla ya kuchezwa tena wikiendi iliyopita, kila timu ilikuwa ilikuwa imepata ushindi mara 106.
Hata hivyo, zipo mechi tano za El Classico zinazotajwa kuwa ndizo za moto zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la Hispania. Ni zipi hizo? Makala haya yanachambua.
Madrid 2-3 Barcelona (Aprili 23, 2017 – La Liga)
Mechi ilichezwa Santiago Bernabeu na wenyeji walianza kupata bao kupitia kwa kiungo raia wa Brazil, Casemiro, lakini Messi aliisawazishia Barcelona dakika tano tu baadaye.
Ivan Rakitic aliiongezea Barca bao la kipindi cha pili na jahazi la Madrid lilionekana kuzama zaidi baada ya nahodha wake, Sergio Ramos, kulimwa kadi nyekundu baada ya rafu yake kwa Messi.
Hata hivyo, mashabiki wa Madrid waliamka kwenye viti baada ya James Rodriguez kuwafungia bao dakika ya 85. Wakati Madrid wakionekana wameondoka na pointi tatu, Messi alifunga bao sekunde ya mwisho ya mchezo.
Barcelona 3-3 Madrid (Machi 10, 2007 – La Liga)
Hii ilikuwa pale Camp Nou, ambapo Messi alifunga ‘hat-trick’ yake ya kwanza katika maisha yake ya soka. Ni siku ambayo Ruud van Nistelrooy aliifungia mabao mawili Madrid na jingine lilipachikwa na Ramos.
Ni msimu ambao Madrid na Barca walimaliza mbio za ubingwa wakiwa wanalingana pointi (76). Hivyo, Madrid walitwaa ubingwa kwa kanuni ya ushindi walioupata walipokutana na Barca.
Madrid 4-2 Barcelona (Aprili 10, 2005 – La Liga)
Zinedine Zidane aliitanguliza Madrid mwanzoni kabisa mwa mchezo, kisha Ronaldo Nazario akaweka jingine, kabla ya Michael Owen kupachika bao la nne katika dakika ya 65.
Ni siku ambayo Madrid ilijaza mastaa wake wote waliokuwa wamesajiliwa kwa bei mbaya, wakiwamo Beckham, Roberto Carlos, Luis Figo na Iker Casillas.
Katika mchezo huo, Barcelona ilipata mabao yake kupitia kwa Samuel Eto’o na Ronaldinho lakini hayakutosha kuinasua katika kichapo cha ugenini pale Santiago Bernabeu.
Madrid 2-6 Barcelona (Mei 2, 2009 – La Liga)
Gonzalo Higuain aliitanguliza Madrid katika dakika ya 14 ya mchezo lakini Thierry Henry aliisawazishia Barcelona dakika nne tu baadaye.
Kama hiyo haitoshi, Henry aliongeza jingine, kisha Messi naye akafunga mawili, kabla ya mabao mengine mawili kutoka kwa mabeki Carles Puyol na Gerard Pique.
Itakumbukwa, ni msimu ambao Barcelona walitwaa ubingwa wa Ligi [La Liga] wakiwa wameizidi pointi tisa Madrid iliyoshika nafasi ya pili kwenye msimamo.
Madrid 1-0 Barcelona (Aprili 20, 2011 – Copa del Rey)
Ilikuwa ni fainali ya Copa del Rey. Baada ya dakika 90 kumalizika bila kupatikana mshindi [0-0], vita ilihamia kwenye dakika 30 za nyongeza.
Hata hivyo, wakati wengi wakidhani mechi ingesogea hadi kwenye mikwaju ya penalti, Cristiano Ronaldo aliifungia Madrid bao la ushindi, akitumia ‘asisti’ ya winga Angel Di Maria.
Di Maria alitolewa kwa kadi nyekundu dakika chache tu baadaye lakini bao hilo lilidumu na Madrid wakatwaa taji lao la kwanza chini ya kocha raia wa Ureno, Jose Mourinho.


