4.9 C
New York

Waliosoma Nyamburi kujenga maabara tatu za sayansi

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini- Serengeti

ZAIDI ya vijana 90 waliosoma Shule ya Sekondari Nyamburi, wilayani Serengeti, mkoani Mara, wameungana kuchangisha rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa maabara tatu za sayansi zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Vijana hao, wanaotoka katika vijiji vya Bisarara na Nyamburi, Kata ya Sedeco, wameanza kutekeleza mpango huo kwa kuchangia mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya kuanza ujenzi, huku wakitarajia kupata ushirikiano zaidi kutoka kwa wananchi na wadau wengine wa maendeleo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bisarara, Thomas Marwa, amesema Serikali ya Kijiji na wananchi wameunga mkono mpango huo kwa kukubaliana kuchangia mifuko 800 ya saruji, pamoja na vifaa na nguvu kazi zitakazohitajika katika ujenzi wa maabara hizo.

Amesema baada ya vijana hao kuwasilisha mpango wao, vikao vya Serikali ya Kijiji vilifanyika na maazimio kuwasilishwa kwa wananchi kupitia mkutano wa hadhara, ambapo walikubaliana kuchangia vifaa vya ujenzi na gharama za mafundi.

Kwa mujibu wa Marwa, wananchi wamekubaliana kuchangia tripu 21 za mchanga, tripu 19 za kokoto, tripu 14 za mawe pamoja na fedha za kulipia mafundi watakaoshiriki katika ujenzi huo.

Amesema vijana hao, ambao baadhi wameajiriwa serikalini huku wengine wakifanya biashara katika maeneo mbalimbali nchini, wameamua kurudisha fadhila kwa shule waliyosoma kwa kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu.

“Kwa vile vijana hao wanatoka vijiji viwili vya Bisarara na Nyamburi, katika kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Diwani Raphael Matiko, tumekubaliana kugawana majukumu ya ujenzi wakati wa kutekeleza mradi huo kwa kushirikisha wananchi wetu na kuwaeleza uamuzi wa vijana wao kujenga maabara hizo,” amesema Marwa.

Ameongeza kuwa vijana hao wamekuwa wakichangia pia miradi mingine ya maendeleo katika kijiji hicho, akitoa mfano wa mchango wa Sh milioni 1.7 waliotoa kwa ajili ya kununua eneo ambalo kituo cha afya kimejengwa, sambamba na wananchi waliochangia Sh milioni saba.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Sedeco, Raphael Matiko, amewapongeza vijana hao kwa uamuzi wao wa kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu na kupunguza changamoto zinazoikabili shule hiyo, zikiwamo za madarasa na mabweni.

Matiko amesema viongozi wa kata, vijiji na vitongoji wataendelea kushirikiana na wananchi kuwaunga mkono vijana wanaojitokeza kusaidia miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji na barabara.

Amewahimiza vijana wengine kuiga mfano huo kwa kutumia umoja wao na rasilimali walizonazo kuchangia maendeleo ya jamii zao.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamburi, Catherine Beda, amethibitisha kupokea taarifa kuhusu mpango wa ujenzi wa maabara hizo, akisema shule itakuwa tayari kupokea mradi huo baada ya taratibu zinazohitajika kukamilika.

Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuongeza fursa kwa wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi katika mazingira yenye miundombinu inayowawezesha kufanya majaribio ya vitendo, hatua inayoweza kuchangia kuimarisha uelewa na hamasa yao katika masomo hayo.

Related articles

Recent articles