16.8 C
New York

Majizzo awapa changamoto wasanii wa Singeli

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Mkurugenzi wa EFM, Francis Majizzo, amewapa changamoto wasanii wa muziki wa Singeli kuonyesha uwezo wao wa kujaza viwanja, akiahidi kutoa jukwaa na maandalizi ya tamasha litakalofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Kupitia ujumbe wake aliouchapisha leo Ijumaa, Oktoba 16, 2026 katika ukurasa wake wa mtadao wa Instagrama, Majizzo amesema kuwa hatua hiyo inalenga kumaliza malumbano yanayoendelea miongoni mwa wasanii hao, huku baadhi yao wakilalamikia kukosekana kwa matukio makubwa ya muziki huo ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Majizzo amesema anaelewa changamoto zinazowakabili wasanii hao kutokana na kusimama kwa matukio yaliyokuwa yakiwapa fursa ya kujitangaza na kujipatia kipato, yakiwamo Funga Mtaa, Komaa Concert na Muziki Mnene.

Amesema licha ya kutokujibu kauli zinazomhusu binafsi, hatazipuuza hoja zinazohusu maendeleo ya muziki wa Singeli, akibainisha kuwa matukio hayo yalisimama kwa sababu mbalimbali za msingi na yatarejea kwa wakati mwafaka.

Hata hivyo, amewataka wasanii hao kuacha malumbano na badala yake kutumia fursa ya jukwaa kuonyesha uwezo wao mbele ya mashabiki.

“Sasa majibu mtatoa nyie. Mimi nawapa stage, muziki na kila kitu kuandaa event, tarehe 25 mwezi huu wa kumi, nina nafasi,” amesema Majizzo.

Ameongeza kuwa wasanii hao wako huru kuchagua uwanja watakaotaka kufanyia tamasha hilo, huku yeye akiahidi kusimamia maandalizi ya jukwaa na muziki.

“Ninyi chagueni uwanja, nielekezeni nikafunge jukwaa na muziki mnaotaka. Tunapiga Singeli mwanzo mwisho, tujue mkali nani, mthibitishe ufalme wenu wa kitaa,” amesema.

Majizzo amesisitiza kuwa sasa ni wakati wa wasanii hao kujibu hoja zinazotiliwa shaka kuhusu uwezo wao kwa vitendo badala ya kuendeleza mabishano.

“No more words, twende uwanjani,” amehitimisha Majizzo.

Ujumbe wa Majizzo umetolewa saa chache baada ya mmoja wa wasanii wa Singeli kuhoji mchango wake katika kukuza muziki huo, hatua iliyozua mjadala na mvutano mitandaoni, huku baadhi ya wadau wakisisitiza kuwa @majizzo amekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza tasnia ya Singeli.

Related articles

Recent articles