Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini, LATRA, imewataka wasafirishaji nchini kuwa watulivu na kuepuka kupandisha nauli kiholela kutokana na ongezeko la bei za mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, amesema mamlaka hiyo inatambua changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya bei ya mafuta, huku akisisitiza kuwa hatua yoyote ya kuongeza nauli lazima ifuate taratibu rasmi zilizowekwa.
“Tunawaomba wasafirishaji kuwa na subira katika kipindi hiki. Wasipandishe nauli bila kufuata utaratibu rasmi hadi pale tutakapokutana nao na kujadiliana kwa pamoja,” amesema Suluo.
Ameongeza kuwa LATRA imepanga kukutana na wadau wa sekta ya usafirishaji Aprili 8, 2026 ili kujadili mustakabali wa nauli za usafiri wa umma na kufikia muafaka utakaolinda maslahi ya pande zote, wakiwemo abiria na watoa huduma.
Kwa mujibu wa LATRA, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa mabadiliko yoyote ya nauli yanazingatia hali halisi ya uchumi na hayawaumizi wananchi wanaotegemea usafiri wa umma katika shughuli zao za kila siku.
Aidha, wananchi wametakiwa kuripoti vitendo vyovyote vya upandishaji holela wa nauli kwa mamlaka husika hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.


