2 C
New York

Mwangwi wa sheria| Mambo usiyoyajua kisheria kuhusu kesi za mauaji-4

Published:

Na Wakili Baraka Asajile Gwakabale

IFAHAMIKE kuwa kukiri kosa hakufungi mjadala wa kisheria. Kukiri kosa ni kitendo cha mshitakiwa kukubali kuwa alihusika katika kitendo cha jinai, lakini kukiri hakufanyi kesi kuisha au kuondoa wajibu wa mahakama kuchunguza ukweli. Sheria inatambua kwamba:

Kukiri kosa kunapaswa kuwa kwa hiari kamili, bila shinikizo, vitisho, au udanganyifu kutoka kwa maafisa wa polisi, familia, au vyombo vingine.

Mahakama inapaswa kuthibitisha kuwa kukiri kulitolewa kwa hiari na mshitakiwa alielewa kikamilifu matokeo ya kitendo chake.

Kukiri kunakochukuliwa bila hiari halina nguvu kisheria. Hii inamaanisha kwamba, hata kama mshitakiwa amesema alihusika, kesi ya mauaji inaweza kuendelea kama ushahidi mwingine unaonyesha hitilafu katika njia ya kukiri.

Kukiri kosa ni moja tu ya vipengele vinavyochukuliwa katika kesi ya jinai. Serikali ina jukumu la kuhakikisha uchunguzi wa kweli unafanywa, ushahidi unakusanywa kwa usahihi, na haki za wahasiriwa na mshitakiwa zinaheshimiwa kikamilifu.

Kwa upande mwingine, ushahidi wa mazingira unaweza kumtia mtu hatiani. Ushahidi wa mazingira ni ushahidi unaotokana na hali, matukio, au vitu vilivyopo kwenye mahali pa tukio, na siyo ushahidi wa mtu binafsi (shahidi wa macho). Hii inaweza kujumuisha alama za vidole, damu, silaha, rekodi za kielektroniki, au hali ya mahali pa tukio.

Sheria inatambua kwamba Mahakama inaweza kuchukua uamuzi bila shahidi wa macho, mradi tu ushahidi wa mazingira unaonyesha kwa uwazi matokeo ya tukio na unaunda picha kamili ya kutosha ya hatia.

Vilevile, ushahidi huu lazima ujenge hitimisho lisiloacha shaka ya hatia. Hii ni kanuni ya jumla ya jinai inayosema kuwa mshitakiwa hatoweza kuhukumiwa kwa dhana; lazima kuwe na ushahidi unaothibitisha hatia kwa kiwango cha juu zaidi kinachohitajika kisheria.

Kama hiyo haitoshi, ushahidi wa mazingira unaweza kuunga mkono au kuthibitisha ushahidi mwingine. Hata kama kuna mashahidi wa macho, ushahidi wa mazingira husaidia kuthibitisha hadithi zao na kuondoa migongano au utata.

Isisahaulike pia, umri wa mtuhumiwa una athari kisheria. Kifungu husika hapa ni cha 15 na 26(2). Mtoto chini ya umri fulani hawezi kuwajibika kikamilifu, na adhabu ya kifo haitolewi kwa aliyekuwa chini ya miaka 18 wakati wa kosa.

Umri wa mtuhumiwa ni kipengele muhimu kinachoathiri uwezo wake wa kuwajibika kisheria. Sheria inatofautisha kati ya watoto, vijana, na watu wazima katika kushtakiwa kwa makosa ya jinai, hasa makosa makubwa kama mauaji.

Itaendelea…Mawasiliano: – 0784745645

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img