7.9 C
New York

Maisha, mikasa ya Bob Marley (2)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA chapisho lililopita, ambalo ni sehemu ya kwanza ya Simulizi ya maisha ya gwiji wa muziki wa Reggae, Bob Marley, tuliona namna yeye na mama yake walivyohamia na kuanza kuishi nyumbani kwa mwanaume aitwaye Thadeus Livingston.

Kama ilivyosimuliwa, Thadeus alikuwa na mtoto wa kiume, Neville Livingston, ambaye baadaye alifahamika kwa jina la Bunny Wailer.

Wakiwa hapo nyumbani, Wailer na Bob walianza kuonesha uwezo wa kuimba, ambapo walikopi nyimbo za R&B za wanamuziki waliokuwa wakitamba enzi hizo nchini Marekani.

Baadaye, Bob na Wailer walikutana na kijana mwenzao, Peter Tosh, na kuunda Kundi lao la ‘Teenagers’, ambalo lilikuja kuitwa ‘Wailing Rudeboys’, ‘Wailing Wailers’, na mwisowe kuangukia jina la ‘Wailers’.

Wakati huo, si Bob, Wailer wala Tosh aliyekuwa na uwezo wa kutumia zana za muziki, na badala yake wote walikuwa waimbaji tu.

Jirani na walikokuwa wakiishi Bob na Wailer, aliishi pia jamaa aitwaye Joe Higgs, ambaye anatajwa kuwa ndiye aliyewafundisha ucharazaji wa nyuzi za gitaa.

Miaka ikaenda na hatimaye mama yake Bob, Cedella, akaachana na Thadeus na kuolewa na Edward Booker, ambaye alikuwa mtumishi wa Serikali ya Marekani. Walibahatika kupata watoto wawili; Richard na Anthony.

Februari 1962, Bob aliachia ngoma nne, ambazo ni ‘Judge Not’, ‘One Cup of Coffee’, ‘Do You Still Love Me?’ na ‘Terror’, prodyuza akiwa ni Leslie Kong.

Hata hivyo, wimbo uliowaweka kwenye ramani ni ‘Simmer Down’, ambao waliutoa kupitia Kundi la Wailers lililokuwa na jumla ya wasanii sita (Bob, Wailer, Tosh, Braithwaite, Kelso na Smith).

Ni baada ya wimbo huo kushika namba moja katika chati za muziki nchini Jamaica na kuuza nakala zaidi ya 700,000, ndipo Waillers ilipoanza kufanya kolabo na wasanii wakubwa wa Jamaica, wakiwamo Ernest Ranglin, Jackie Mittoo na Roland Alphonso.

Mwaka 1966, Wailers ilitikiswa kidogo na kitendo cha Braithwaite, Kelso na Smith kuondoka kundini, hivyo kuwaacha Bob, Wailer na Tosh wakiendeleza harakati.

Ni kipindi hicho, Bob alifunga ndoa na mrembo Rita Anderson na mwanamuziki huyo kuhamia Delaware, Marekani, jirani na alikokuwa akiishi mama yake baada ya kuolewa na mtumishi wa Serikali, Booker.

Aliporejea Jamaica, ndipo Bob alipoanza kuifuata imani ya Kirastafari, licha ya kwamba amezaliwa na kukulia katika mafundisho ya Dini ya Kikiristo.

Mwaka 1969 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Waillers baada ya kukutana na prodyuza mkongwe wa Reggae, Leslie Kong, ambaye aliwaunganisha akina Bob na Kundi lake la Beverley’s All-Stars.

Wakati wa kurekodi, Kundi hilo liliwasaidia akina Bob katika upigaji wa ala za muziki na ndipo zilipozalishwa ngoma kali, zikiwamo ‘Soul Shakedown Party’, ‘Stop That Train’, ‘Caution’, ‘Go Tell it on the Mountain’, ‘Soon Come’ ‘Can’t You See’, ‘Soul Captives’, ‘Cheer Up’, ‘Back Out’ na ‘Do It Twice’.

Unajua nini kilifuata? Tukutane hapa Jumamosi ijayo kwa mwendelezo wa maisha na mikasa ya Bob Marley.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img