3.2 C
New York

Kuelekea Uchaguzi Mkuu Uganda 2026

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

UCHAGUZI Mkuu wa Uganda unatarajiwa kufanyika Januari 15, mwakani, ambapo Rais Yoweri Museveni anawania muhula wake wa saba madarakani.

Wakati Rais Museveni akiwa ameiongoza Uganda kwa miaka 40, safari hii mpinzani wake mkubwa ni Bobi Wine, licha ya kuwapo kwa wagombea wengine sita kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Wapinzani, akiwamo Bobi, wanalalamikia ‘rafu’ wanazochezewa na Rais Museveni, ikiwamo mikutano yao ya kampeni kuingiliwa na vyombo vya dola na wakati mwingine matumizi makubwa ya nguvu dhidi yao.

Kwa mujibu wa Katiba, mshindi wa kiti cha urais anapaswa kufikisha asilimia 51 ya kura, vinginevyo Uchaguzi utarudiwa.

Takwimu zinaonesha kuwa wananchi zaidi ya milioni 18 wameshajiandikisha kwa ajili ya kupiga kura. Ni katika taifa lenye watu milioni 46.

Kati yao, vijana wenye umri chini ya miaka 30 waliojiandikisha ni milioni 10.7). Ni sawa na asilimia 32.4 ya idadi ya vijana wote milioni 33.

Uchaguzi uliopita wa mwaka 2021 uligubikwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kutekwa kwa wafuasi wa vyama vya upinzani takribani 3,000.

Katika matukio mengine, vyombo vya dola vilitumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha kutawanya mikutano ya kampeni ya upinzani.

Dosari hizo zimejitokeza pia kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Kwa sasa, mamia ya wafuasi wa upinzani wanashikiliwa na vyombo vya dola.

Kwa mujibu wa kile kinachoelezwa na ripoti ya Umoja wa Mataifa, wafuasi zaidi ya 550 wamekamatwa tangu mwaka huu ulipoanza. Wengi ni baada ya mikutano ya kampeni kuanza Septemba.

Licha ya mazingira magumu hayo, bado Bobi Wine ndiye mgombea wa urais anayetajwa ‘kumpasua kichwa’ Rais Museveni zikiwa zimebaki wiki chache kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Ni kama ilivyokuwa katika Uchaguzi uliopita wa mwaka 2021, ambapo Rais Museveni alipata ushindi mwembamba wa asilimia 58 ya kura, huku Bobi Wine akikusanya asilimia 35.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img