2.9 C
New York

Ndejembi: Tanzania sasa ina umeme wa kutosha, mgao utabaki historia

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania kwa sasa ina umeme wa kutosha, na kwamba ukamilifu wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) umeondoa kabisa mgao wa umeme nchini.

 Ndejembi ameyasema hayo leo, Novemba 26, 2025, wakati wa ziara yake katika Mradi wa JNHPP, iliyo­lengwa kujionea namna uzalishaji unavyoendelea na kuthibitisha ufanisi wa mradi huo.

Amesema mradi huo tayari umekamilika na una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, kiwango ambacho kimeleta uthabiti wa upatikanaji wa nishati na kupunguza changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo nchini.

“Tangu uzalishaji ulipoanza hapa, kumekuwa na maboresho makubwa katika usambazaji wa umeme. Sasa Serikali inajikita kwenye ujenzi wa njia za kusambaza nishati ili kuufikisha katika maeneo mengi zaidi,” amesema Waziri Ndejembi.

Amefafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na unaendelea kuzalisha umeme kwa ufanisi.

Akizungumzia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, Waziri Ndejembi amesema kazi inaendelea, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha upatikanaji wa nishati katika mikoa ya Kati, Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Aidha, amesema Serikali ipo kwenye hatua za kuanza ujenzi wa njia nyingine muhimu ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Mkuranga, ambayo itapeleka nishati katika Kongani ya Viwanda Mkuranga na kulilisha Jiji la Dar es Salaam.

Amesema uhai wa mradi huo unategemea utunzaji wa rasilimali maji, ambapo asilimia 80 ya maji ya bwawa yanatoka Mto Kilombero na asilimia 20 kutoka Mto Ruaha na mito mingine midogo. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maji, Maliasili na Utalii, Mifugo pamoja na TFS kulinda vyanzo vya maji.

Ameeleza kuwa endapo vyanzo hivyo vitatunzwa ipasavyo, Tanzania inaweza kupata umeme wa uhakika kwa zaidi ya miaka 100 kupitia mradi wa Julius Nyerere. Amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuulinda na kuuthamini mradi huo kwa manufaa yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Bw. Lazaro Twange, amesema uwekezaji unaoendelea katika miradi ya umeme umefikia Shilingi trilioni 13.5.

Amebainisha kuwa kati ya miradi 41 inayoendelea, sita ni ya uzalishaji na 35 ni ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme.

“Kwa sasa Tanzania ina umeme wa ziada na hakuna mgao. Matangazo yanayotolewa ya kuzimwa kwa baadhi ya maeneo kwa muda mfupi ni kwa ajili ya maboresho ya miundombinu,” amesema Twange.

Ameongeza kuwa Tanesco inaendelea kuboresha upatikanaji wa nishati katika maeneo ya viwanda, ikiwemo ujenzi wa njia ya umeme kutoka Mkuranga kuelekea Chalinze, Kibaha na Kwala, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 3 zimewekezwa ili kuhakikisha viwanda vinapata umeme wa uhakika.

Amesisitiza kuwa miradi mipya ya umeme wa jua na maji inaendelea, ikiwemo Mradi wa Kishapu mkoani Shinyanga (MW 50) na Malagarasi Kigoma (MW 49.5), ambayo itaunganishwa kwenye gridi ya taifa hivi karibuni.

Akizungumzia agizo la Rais kuhusu maandalizi ya kuzalisha umeme wa nyuklia, Twange amesema mazungumzo yanaendelea na wawekezaji mbalimbali, huku Wizara ya Nishati ikiwa katika hatua za mwisho za maandiko ya awali kabla ya vikao vya wadau kuanza.

Amesema Tanzania ina umeme wa kutosha, hivyo mwekezaji yeyote anakaribishwa kuwekeza nchini kwani Tanesco iko tayari kutoa huduma bila changamoto ya upungufu wa nishati.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa mikutano ya Waziri wa Nishati kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake ili kufahamu namna zinavyotekeleza majukumu yao.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img