4.1 C
New York

Kane akanusha kurudi England, ataka mkataba Bayern

Published:

MUNICH, Ujerumani
MPACHIKAJI mabao wa Bayern Munich, Harry Kane, amesema si kweli kwamba atarudi Ligi Kuu ya England, na badala yake anataka kusaini mkataba mpya Allianz Arena.
Kane amebakiza miezi 24 katika mkataba wake wa miaka minne aliosaini baada ya kutua Bayern mwaka 2023 akitokea Tottenham kwa ada ya Pauni milioni 86.4.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32, amefunga mabao 103 katika mechi 106 alizocheza akiwa na jezi za Bayern ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).
Msimu uliopita, alikiongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Bundesliga, likiwa ni taji lake kubwa la kwanza katika maisha yake ya soka.
Hivi karibuni, kocha mpya wa Tottenham, Thomas Frank, alisema atafurahi kuona Kane anarejea katika klabu hiyo ya Kaskazini mwa Jiji la London.
Muingereza huyo aliondoka Tottenham akiwa amebakiza mabao 48 pekee kufikia rekodi ya Alan Shearer, ambaye kwa sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu ya England akiwa na mabao 260.
Hata hivyo, Kane ambaye ndiye nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya England, amesema hana mpango huo.
“Kwa ishu ya kubaki hapa kwa muda mrefu, hakika ningependa iwe hivyo. Sijajua kuhusu kurudi England, lakini kama nitaambiwa nichague, basi nitachagua kubaki Bayern,” alisema.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img