Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dk. Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili itakayoanza kesho Mei 20-21,2025 kwa mualiko wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Shaaban Kissu imesema ziara hiyo ni ya kwanza kwa Rais huyo tangu alipoapishwa Machi 21,2025, ikilenga kukuza ushirikiano wa kiasiasa, kiuchumi na kijamii ikiwamo nyanja za biashara, uwekezaji na elimu.
Imesema Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kidugu na kidiplomasia,hivyo ziara hiyo itafungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowawezesha wananchi wa nchi zote mbili kunufaika kiuchumi.

Rais Dk. Nandi-Ndaitwah atapokelewa Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Samia ambapo viongozi hao wawili wanatarajia kuwa na mazungumzo na baadae kuzungumza na waandishi wa habari.
Aidha, akiwa nchini Tanzania, Rais huyo atatembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama sehemu ya kuthamini mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi barani Afrika.


