1.7 C
New York

GGML yatoa elimu ya haki, wajibu maadhimisho Siku ya Mtoto wa Afrika

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

KATIKA kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeshirikiana na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi kitengo cha dawati la jinsia pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kutoa elimu mbalimbali juu ya haki na wajibu wa mtoto katika jamii katika maeneo yanayozunguka mgodi ikiwemo Bugulula, Kasota na Nyawilimilwa.

Katika maadhimisho hayo ambayo hufanyikaJuni 16, ya kila mwaka, GGML imefanya kampeni mbalimbali kutoa elimu juu ya haki za mtoto wa Afrika na wajibu wake ndani ya jamii.

Rebbeca Manace kutoka Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia mkoani Geita akitoa elimu juu ya haki za Watoto.

Akizungumza mjini Geita kwa niaba ya GGML Meneja mwandamizi anayesimamia mahusiano ya jamii kutoka GGML, Gilbert Mworia amesema kuwa watoto ni sehemu muhimu katika jamii ambayo inapaswa kushirikishwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

“Siku ya mtoto wa Afrika ni muhimu kwa kila mmoja wetu kwa kuwa inatukumbusha umuhimu wa kundi hili ndani ya jamii yetu. Watoto ni taifa la sasa na kesho, tunapaswa kuwalinda kwa kuwapatia haki zao za msingi ikiwemo elimu. 

“GGML itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye kuwanufaisha watoto ndani ya mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla ikiwemo ujenzi wa shule, vituo vya afya, miundombinu na miradi endelevu yenye tija kwa maendeleo endelevu,” amesema akitoa wito kwa wazazi na walezi kutoruhusu watoto kuingia maeneo ya migodi kutafuta kipato kwa kuwa ni mazingira hatarishi.

Akitoa elimu kwa watoto na wazazi katika Shule ya Msingi Kamlale iliyopo kata ya Nyawilimwila katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Rehema Kabanda amesema kuwa serikali itaendelea kuhamasisha matumizi bora ya kidigitali ili kumwepusha mtoto na masuala yasiyo na tija katika jamii.

“Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika inasisitiza kuzingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidigitali.Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuwaongoza vyema watoto wao juu ya matumizi salama ya kidigitali kwa kuwa ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii na kuathiri maendeleo yetu wote,” amesema Rehema Kabanda.

Siku ya Mtoto wa Afrika ni siku inayosherehekewa kila mwaka tarehe 16 Juni, ilianza kuadhimishwa mwaka 1991 ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano katika mji wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 pamoja na kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto.

Katika siku hiyo, maelfu ya watoto katika nchi ya Afrika Kusini walikusanyika katika mji wa Soweto kwa ajili ya maandamano yenye malengo ya kudai elimu bora. Mamia ya watoto walipigwa risasi na kuuliwa wakati watoto zaidi ya elfu moja walijeruhiwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img