22.9 C
New York

Infographic| Hali ilivyo Uturuki, Syria baada ya matetemeko ya ardhi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Watu 7,266 wameripotiwa kupoteza maisha huku wengine 35,626 wakijeruhiwa kufuatia matetemeko ya ardhi yaliyozikumba nchi za Uturuki na Syria usiku wa Jumatatu ya Februari 6, 2023.

Kwa upande wa waliopoteza maisha hadi usiku wa Februari 7, saa 5:50 watu 5,434 walikuwa wamepoteza maisha upande wa Uturuki huku Syria wakiwa 1,832.

Upande wa majeruhi Uturuki ameripoti kufikia watu 31,777 huku Syria wakiwa 3,849.

Aidha, matetemeko hayo ambayo lakwanza lilianza saa 10:17 Alfajiri ya Februari 6 likiwa na ukubwa wa 7.8 na jingine lililofuatia saa 7 mchana likiwa na ukubwa wa 7.5, yameharibu majengo 5,775 nchini Uturuki.

Sambamba na hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limearifu kuwa zaidi ya watu milioni 3 wameachwa bila makazi ambapo kati yao watoto ni milioni 1.

Tayari Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ametangaza hali ya dharura ya miezi mitatu katika mikoa 10 iliyotikiswa na matetemeko mawili ya ardhi.

Siku moja baada ya matetemeko hayo kutikisa Uturuki na Syria, waokoaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu wanapambana kuwaondoa watu kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Hali ya hewa ya baridi kali imeathiri juhudi za uokozi na upelekaji misaada, na baadhi ya maeneo hayana nishati.

Katika hotuba yake ya Februari 7, mwaka huu, Rais Erdogan amesema mikoa 10 ya nchini Uturuki imeathirika kama eneo la mkasa huo na akatangaza hali ya dharura katika jimbo hilo kwa miezi mitatu.

Timu za uokozi kutoka karibu nchi 30 kote ulimwenguni zinaelekea Uturuki au Syria huku ahadi za msaada zikiendelea kumiminika.

Uturuki imesema itayaruhusu tu magari yaliyobeba misaada kuingia katika mikoa iliyoathirika kabisa ya Kahramanmaras, Adiyaman na Hatay ili kuharakisha shughuli za utafutaji na uokozi.

Umoja wa Mataifa umesema unatafakari mbinu zote za kufikisha msaada kaskazini magharibi mwa Syria, ambako mamilioni ya watu wanaishi katika kiwango kikubwa cha umaskini na hutegemea msaada wa kiutu ili kuishi.

Aidha, tayari Umoja wa Ulaya umetuma timu 27 za uokozi kutoka nchi 19 kusaidia kuwatafuta manusura nchini Uturuki.

Vitengo hivyo vinajumuisha wafanyakazi 1,150 wa uokozi na mbwa 70. Hii leo, Australia na New Zealand ni miongoni mwa nchi za karibuni kabisa kuahidi msaada nchini Uturuki na Syria.

Rekodi zinaonyesha kuwa hadi sasa madhara ya matetemeko hayo yanashika nafasi ya 11 nyuma ya madhara mengine 10 yaliyowahi kutokea duniania huku kubwa likiwa lile la mwaka 2010 lililoikumba nchi ya Haiti ambapo watu 222,570 walipoteza maisha.

Endelea kusoma www.gazetini.co.tz kwa ajili ya taarifa zaidi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img