1.6 C
New York

Serikali na mkakati wa kusajili watoto wote nchini

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

SERIKALI imeagiza kusajiliwa kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano na kwamba huduma hiyo inatolewa bure.

Wito huo umetolewa Juni 3, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo wakati akizindua Mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika mkoa wa Tabora, ambapo hadi sasa Mikoa 22 nchini imenufaika na mpango huo tangu ulipozinduliwa nchini mwaka 2013.

Mpango huo unatekelezwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo una lengo la kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini.

Mbali na kufungua mlango wa haki ya kutambuliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, mpango huo umekuwa na matokeo makubwa ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili Serikali na wananchi kuhusiana na usajili wa vizazi.

“Lazima tutambue kuwa cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila mtoto aliyezaliwa katika ardhi ya Tanzania awe raia na asiye raia, kinachotakiwa ni wazazi wa mtoto husika kuthibitisha uraia wao kabla taratibu za kumsajili mtoto hazijaanza.

“Hivyo niwatake wananchi kutoa msaada na ushirikiano katika zoezi la utambuzi wa wazazi wenye sifa za kusajili watoto wenu ili wapewe vyeti vya kuzaliwa,” amesema Makondo.

 Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Angela Anatory akizungumza mapema mweiz huu kuhusu Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano katika mkoa wa Tabora amesema lengo lake ni kuhakikisha kila mtoto ambae hajasajiliwa, anasajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa.

Aidha, amesema mpango huo utahakikisha kwamba kila mtoto atakayezaliwa kuanzia siku Mpango huo umeanza kutekelezwa anasajiliwa ndani ya muda mfupi baada ya tukio la kizazi kutokea.

“Chimbuko la mpango huu ni uwepo wa kiwango kidogo cha wananchi ambao wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hapa nchini kutokana na sababu mbalimbali zilizosababisha wananchi kushindwa kusajili vizazi hivyo basi serikali na wadau kuamua kubuni Mpango huu unaoenda kutatua changamoto zilizopo katika mfumo wa awali.

“Mpango wa Usajili wa Watoto unaleta maboresho yafuatayo katika Mfumo wa Usajili; moja, kusogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi na huduma kupatikana katika vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto na katika Ofisi za Watendaji Kata.

“Pili, kuondoa ada ya cheti kwa watoto wanaosajiliwa kupitia Mpango huu hivyo nyaraka hiyo kutolewa BILA MALIPO. Tatu, kuimarisha mfumo wa kutuma na kuhifadhi taarifa za waliosajiliwa kwa kutumia TEHAMA ambapo simu ya kiganjani iliyowekwa programu maalum hutumika,” amesema Anatory.

Kwa muji wa Anatory, mpango huo mpaka sasa umeanza kutekelezwa katika mikoa 22 ya Mwanza, Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Geita, Shinyanga, Lindi, Mtwara, Simiyu, Morogoro, Pwani, Mara, Dodoma, Singida, Ruvuma, Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Rukwa na Katavi.

“Kwa ujumla Mafanikio ya utekelezaji wa Mpango huu katika mikoa iliyotangulia ni makubwa na mpaka sasa zaidi ya watoto 7,549,878 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa,hivyo kuongeza kiwango cha usajili kutoka asilimia 13 mwaka 2012 na kufikia asilimia 65 mwaka 2021.

“Hii ni sawa na kusema kwamba zaidi ya nusu ya watoto nchini wamepata haki yao ya msingi ya kutambuliwa na taarifa zao kuingizwa katika mfumo rasmi wa utambuzi wa serikali,” amesema Anatory.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img