4.1 C
New York

Serikali, wataalamu wa nishati jadidifu kuwawezesha wanahabari kuripoti maswala ya nishati safi kwa weledi 

Published:

Na Tulinagwe Malopa, Gazetini

Wakati wiki ya kwanza ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP27 ukiendelea Sharm el-Sheikh nchini Misri, Novemba 9 & 10,2022 wanahabari na wataalamu wa maswala ya Nishati Jadidifu walikutana jijini Dar es Salaam ili kujibu maswali muhimu kuhusu mchango wa wanahabari katika sekta hio ikiwemo namna wanahabari wanavyoweza kujinoa kuandika habari hizo kwa weledi. 

Baadhi ya Waandishi wa habari walioshiriki katika mafunzo ya nishati jadidifu.

Shirika lisilo la kiserikali la TaTEDO kwa kushirikiana na WWF wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanahabari wanapata uelewa wa namna ya kutengeneza maudhui bora na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa matumizi bora kupitia vyanzo sahihi visivyo na madhara kwa mazingira.

Mkururugenzi Mtendaji wa wa Tatedo, Estomih Sawe amesema kama wanahabari ni vyema tukijiweka karibu na wadau mbalimbali wanaojihusisha na teknolojia zinazolenga kutunza mazingira ili kusukuma gurudumu la maendeleo pamoja. 

“Hatuwezi kufanya kazi hii wenyewe ndio maana kama wadau wa maswala haya tunajaribu kutafuta njia za kufanikisha lengo letu ikiwemo kushirikiana na wanahabari,” amesema Sawe. 

Amesema kuna haja ya kuwahamasisha wananchi na kuwaelimisha ili wafahamu kuwa kuna nishati safi ambazo unaweza kutumia badala ya mkaa na ukapika chakula kwa bei nafuu, haraka na kwa usalama.

“Tunataka kuwakikishia kuwa lazima tuhamie teknolojia nyingine ya kupikia joto badala ya moto na natoa wito kwa Serikali na wananchi tushirikiane kuhusu kujua umuhimu wa kuwa na nishati mbadala katika kupikia na  upo uwezekano wa kupika kwa kutumia joto badala ya moto kwa ufanisi mkubwa na usiharibu mazingira,” amesema Sawe.

TaTEDO wamebuni teknolojia rahisi za kupikia majumbani ili kuwawezesha watu hasa wanawake kutumia nishati safi na salama ya kuboresha maisha yao.

Moja ya teknolojia hizo ni matumizi ya majiko yanayotumia kiasi kidogo cha umeme (electric pressure cookers (EPCs)). Majiko hayo licha ya kuwa bado hayatumiki sana kwenye jamii kutokana na uelewa mdogo lakini yameonyesha ufanisi mzuri wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Nchini Tanzania, majiko hayo yamekuwa yakizalishwa na kampuni ya huduma za nishati endelevu (Sescom) iliyo chini ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Uhifadhi ya Mazingira (Tatedo).

Serikali kupitia mkuu wa kitengo cha Mazingira, wizara ya Nishati imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau ikiwemo kuandaa mkakati wa kitaifa wa Nishati jadidifu itakayokua tayari mwaka 2023

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img