LONDON, Uingereza
UTAFITI wa hivi karibuni umedai kuwa asilimia 94 ya klabu za soka za Ligi Kuu ya England [EPL] hazipati faida, na badala yake zinajiendesha kwa hasara, na nyingi zina madeni mengi na makubwa.
Hata hivyo, si England pekee, kwa sasa Barcelona ndiyo klabu ya soka hali mbaya ya madeni kwani inadaiwa euro bilioni 2.7.
Kwa miaka mitatu ya hivi karibuni, bajeti ya mishahara ya wachezaji imepanda kwa asilimia 61. Katika msimu wa 2019-20, ilipata hasara ya euro milioni 43. Kiwango hicho kiliongezeka na kufikia euro milioni 56 msimu uliofuata.
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa anguko la kiuchumi la Barcelona lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na usajili wa bei mbaya wa Philippe Coutinho, Ousmane Dembele na Antoine Griezmann.
Man United nayo inashika nafasi ya pili kwa ‘kupumulia mashine’ kiuchumi. Deni la mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya England ni Pauni bilioni 1.15.
Tottenham ni klabu nyingine yenye hali mbaya. Moja ya sababu za uchumi wake kuyumba ni ujenzi wa uwanja mpya uliogharimu Pauni bilioni 1.2. Kwa sasa, deni la klabu hiyo limefikia Pauni milioni 831.2.
Washika Bunduki wa London, Arsenal, licha ya ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, wanafuata katika nafasi ya nne wakiwa na deni la Pauni milioni 426.9.
Chelsea nayo ina madeni ya kutosha. Aprili, 2026, klabu hiyo ya jijini London ilitangaza hasara ya Pauni milioni 262.4. Kampuni inayoimiliki klabu hiyo, BlueCo, nayo ina deni la Pauni bilioni 1.39.
Nje ya England, klabu za Inter Milan, Roma na Juventus nazo ziko hoi. Mathalan, deni la Inter ni Pauni milioni 336, ikifuatiwa na Roma [Pauni Mil. 348.4].


