Na Editha William, Gazetini – Kagera
MKUU wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Siima, amehitimisha rasmi mafunzo ya Jeshi la Akiba [Mgambo] ‘intake’ ya 30/26, yaliyofanyika katika Uwanja wa Kahororo, Kata ya Kashai.
Mafunzo hayo yaliyoanza Juni 29, 2026, yamehitimishwa jana Novemba 6, 2026, ambapo vijana 92 – wanaume 74 na wanawake 18 walihitimu – yalilenga kuwajenga uwezo, nidhamu, uzalendo na kuwaandaa kushiriki shughuli za kijamii na maendeleo, pamoja na kujitengenezea fursa za kujiajiri.
Aidha, Siima amewataka wahitimu hao kuwa wazalendo wa kweli, wenye nidhamu na kujitoa katika kutekeleza majukumu yao ya kijamii kwa kutumia vyema maarifa na ujuzi walioupata wakati wa mafunzo.
Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa wahitimu hao kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo, kuzingatia maadili na kuwa raia wenye uwajibikaji kwa taifa lao.
“Mnapaswa kutumia mafunzo mliyoyapata kwa tija, kudumisha uzalendo na kuwa mfano bora katika jamii kwa kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na kujituma katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” amesema.


