BEIJING, China
TELEVISHENI ya Taifa ya China [CCTV] halikurusha mechi ya Ligi Kuu ya Hispania [La Liga] iliyozikutanisha Real Madrid na Racing Santander iliyochezwa jana Novemba Mosi, 2026.
Mgomo huo ulitarajiwa kwani China imeingia kwenye mzozo mkali na straika wa Madrid, Kylian Mbappe, licha ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kuomba radhi.
Mbappe ameingia kwenye ‘bifu’ na Wachina baada ya kile kilichotafsiriwa kuwa ni kauli ya kejeli aliyoitoa juu ya muasisi wa Taifa lao, Mao Zedong.
Katika picha iliyohaririwa huko mitandaoni, Mbappe aliwekwa kwenye mwonekano wa Zedong, na ndipo nyota huyo alipokomenti kwa kumwita ‘dikteta’.
Kauli hiyo aliyodai kuwa ni utani na kisha kuomba radhi, iliwakera wananchi wengi wa China, hivyo CCTV kuripotiwa kuwa ingegomea kuonesha mechi zote za La Liga.
Katika taarifa yake ya kuomba radhi, Mbappe alisema: “Komenti yangu ilitafsiriwa vibaya na sasa nimegundua kuwa imewaumiza watu wengi wa China na jamii ya Kichina ulimwenguni kote.”


