Na Hassan Mwasha, Gazetini
WEKUNDU wa Msimbazi wameangukia Kundi C msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo watakwaana na vigogo wa Morocco na Afrika Kusini, RS Berkane na Orlando Pirates, na Colombe Sportive ya Cameroon.
Je, ni rahisi kiasi gani kwa Wekundu wa Msimbazi kuvuka kwenye Kundi hilo? Makala haya yanachambua timu zilizoshikilia hatima ya Simba kwenye hatua hii ya makundi msimu huu wa 2026-27.
RS BERKANE
Katika mechi za mashindano za Shirikisho la Soka barani Afrika [CAF], Simba imekutana mara nne na vigogo hao wa Morocco. Kwa mujibu wa takwimu, Simba imefungwa mbili, imeshinda moja na kutoa sare moja.
Mwaka jana [2025], timu hizo zilivaana mara mbili. Katika fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho [Mei 25, 2026], RS Berkane ilishinda mabao 2-0. Fainali ya pili [Mei 25, 2026] ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na Berkane wakawa mabingwa.
ORLANDO PIRATES
Ni mechi ya kibabe. Simba inakutana kwa mara ya tatu na Orlando katika mechi za ushindani. Katika mechi mbili zilizopita, hakuna aliyetamba kwani kila timu ilishinda mara moja.
Mechi ya kwanza ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho ni ile ya Aprili 17, 2022, ambapo Simba ikiwa nyumbani ilishinda bao 1-0, mfungaji akiwa ni beki wa kulia, Shomari Kapombe.
Katika robo fainali ya pili, Simba ikiwa ugenini katika Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini, ilifungwa bao 1-0 na Orlando kusonga mbele [nusu fainali] kwa mikwaju ya penalti [4-3].
COLOMBE SPORTIVE
Wekundu wa Msimbazi watakutana kwa mara ya kwanza na timu hiyo ya Cameroon. Hii pia ni mara yao ya kwanza kuvuka hatua za awali na kuingia makundi kwenye michuano ya CAF.
Hata hivyo, bado Simba hawapaswi kuipuuza Colombe Sportive kwani walifika hatua hii ya makundi kwa kuiondosha Stade Malien ya Mali na Teungueth FC ya nchini Senegal.


