Na Hassan Mwasha, Gazetini
KAMA utataja vichwa vilivyowahi kusumbua kwenye muziki wa kizazi kipya hapa nchini [Bongo Fleva], hutoacha kumtaja Suma Shija Nolobi, maarufu kwa jina la Suma Mnazaleti.
Miaka kadhaa iliyopita, ngoma yake ya ‘Chukua Time’ aliyompa kolabo Ommy Dimpoz, ilikuwa kubwa na kupata muda mwingi wa kuchezwa kwenye vituo vya redio na televisheni.
Baada ya mafanikio makubwa, ikiwamo ngoma nyingine kali ya ‘Hisia za Mtaa’ aliyomshirikisha Steve R&B, ukimya ukatawala na Mnazaleti akapotea mazima kwenye muziki na tasnia ya burudani kwa ujumla. Akawa hasikiki na hakuna aliyekuwa akimuulizia wala kutaka kujua aliko.
Kwa sasa, Mnazaleti amerudi kwa ‘spidi’ kali. Safari hii, si tena kama mwanamuziki, bali amekuja kwa kishindo akiwa na sura mpya kabisa. Alianza kama mchambuzi wa muziki wa Bongo Fleva lakini sasa amejiweka wazi kuwa yeye ni ‘chawa’ wa supastaa Diamond Platinumz.
Turudi nyuma kidogo. Wakati Mnazaleti anatamba na wimbo Chukua Time, Diamond alikuwa ‘mavumbini’ akiwa hana wazo kwamba kuna siku huyo staa angekuja kuwa chawa wake. Maisha bwana!
Mnazaleti amejivua akili ambayo ingemfanya aone aibu kujishusha mbele ya Diamond. Ameamua kuiacha nyuma historia ya ustaa wake, tofauti na binadamu wengi ambao huiishi jana huku wakijua wazi kwamba haiwezi kurudi.
Ni staili ile ile aliyoitumia Baba Levo, ambaye naye alikuwa staa wakati Diamond akiwa hajulikani, lakini alijisogeza karibu yake na kuwa chawa wake. Kupitia njia hiyo, amenufaika pakubwa kupitia Diamond.
Hii ina maana gani? Kwanza, Mnazaleti na Baba Levo ni somo zuri na kubwa kimaisha. Kwamba nafasi au hali uliyonayo inaweza isiwe ya kudumu. Pili, kama huwezi kumpa mkono na kumvuta, basi usimkanyage aliye chini yako maana huwezi kujua kesho yako na yake.


