Na mwandishi wetu, Gazetini
MWAKA 1960, mwanasayansi mmoja alibashiri kuwa dunia itafikia ukomo ifikapo Novemba 13, 2026. Ubashiri huo ulifanywa na mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Illinois, Heinz von Foerster.
Kabla ya msomi huyo, mchumi wa Uingereza, Thomas Malthus, naye aliwahi kuja na ubashiri kama huo.
Malthus alijenga hoja kwamba idadi kubwa ya watu ingeongezeka, kisha kuzalisha janga la njaa, ambalo lingeifanya dunia ifikie ukomo.
Hata hivyo, Von Foerster alipingana na Malthus akisema njaa isingekuwa chanzo cha dunia kufikia mwisho, bali idadi ya watu ingeongezeka na kufikia kiwango kisichodhibitikia.
Von Foerster alisema: “Wajukuu wetu watakufa si kwa sababu ya njaa, bali kutokana na mrundikano wa watu, ambao ungeathiri uwezo wa kupumua na kusababisha vifo.”
Hivyo, alibashiri kuwa dunia ingekuwa kwenye hali mbaya hiyo mwaka 2026, ambapo tayari idadi ya watu imefikia bilioni 8.3.
Idadi ya watu kuongezeka imeanza kuonekana kwenye baadhi ya nchi duniani, zikiwamo Korea ya Kusini na Japan, ambako imekuwapo mikakati ya kuzuia kuzaliana.
Lakini, bado ongezeko la idadi ya watu halionekani kuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya mataifa, ikiwamo Marekani, ambayo Rais wake, Donald Trump, ametangaza zawadi kwa familia kwa kila mtoto atakayezaliwa.
Kama hiyo haitoshi, Rais Trump ameenda mbali zaidi na kutangaza zawadi ya medali kwa mwanamke atayezaa watoto sita au zaidi.
Idadi ya watu duniani ilivuka bilioni moja katika miaka 1800. Kufikia mwaka 1927, idadi hiyo ilishaongezeka mara mbili. Mwaka 1974, idadi iliongezeka tena mara mbili.
Kutoka hapo, ilichukua miaka 13 mingine tu dunia kuwa na watu bilioni tano na mwaka 2022 walishavuka bilioni nane.


