10.4 C
New York

TARURA yajenga barabara za lami karatu, bodaboda waonywa

Published:

Na Catherine Sungura, Tarura

Hata hivyo, waendesha bodaboda wametakiwa kupunguza mwendo kufuatia kuimarika kwa barabara hizo ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo au majeraha.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo, Meneja wa TARURA Karatu, Mhandisi Msetu Madara, amesema wakala huo unasimamia jumla ya kilometa 771 za barabara, zikiwemo kilometa 4.34 za lami zilizopo katika Mji Mdogo wa Karatu, kilometa 315.816 za changarawe na kilometa 451.400 za barabara za udongo.

Amesema TARURA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara za lami ili kuhakikisha miundombinu ya Karatu inaboreshwa na kuwa rahisi kupitika majira yote ya mwaka.

“Wilaya ya Karatu ni mji wa kitalii unaopokea watalii wengi wanaotembelea vivutio kama Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti, hivyo mkakati wetu ni kuhakikisha mji wote unakuwa na barabara za lami,” amesema.

Madara aliongeza kuwa barabara mpya za lami zenye urefu wa kilometa 1.4 zimejengwa pamoja na mitaro ya maji pande zote mbili ili kulinda miundombinu hiyo dhidi ya uharibifu, huku mpango ukiwepo wa kuweka taa za barabarani ili kuimarisha usalama usiku.

Aidha, alisema TARURA imekamilisha ujenzi wa daraja la mawe la Chemchem lenye urefu wa mita 21 na upana wa mita saba katika Kijiji cha Chemchem, likiunganisha vijiji kadhaa vikiwemo Endallah, Manusai, Masabeda, Endamarariek, Basodawishi, Chemchem, Kilimamoja, Gidibaso, Getamock, Qaru na Endabash.

Alisema hadi Februari mwaka huu wakala huo umefanikiwa kujenga madaraja sita ili kuondoa vikwazo vya usafiri na kurahisisha wananchi kupata huduma za kijamii.

Wakati huo huo, TARURA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan waendesha pikipiki kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini Kati, Elisifa Amma, amesema kabla ya ujenzi wa barabara hizo eneo hilo lilikuwa na mashimo na matope yaliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Alisema baada ya ujenzi wa barabara hizo hali imeimarika na shughuli za kiuchumi zimeongezeka, huku akimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu ya mji huo.

Naye mjasiriamali wa mgahawa mjini Karatu, Salome Minja, amesema awali walikosa wateja kutokana na matope na vumbi vilivyosababishwa na ubovu wa barabara.

“Kwa sasa hali imebadilika, mji umechangamka na biashara zinaendelea vizuri. Tunapata wateja wengi zaidi na kipato kimeongezeka,” amesema.

Msimamizi wa miradi hiyo, Mhandisi Daines Simba, amesema ujenzi wa barabara hizo umechochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na kutoa ajira kwa vijana wengi katika kazi za ujenzi.

Naye mkazi wa Chemchem, Philipines Samwuel, amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi walikuwa wakipata shida kuvuka hasa wakati wa masika, lakini sasa usafiri na usafirishaji vinafanyika kwa urahisi mwaka mzima.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img