Na Safina Sarwatt, Gazetini
HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) imeanza ujenzi wa Taasisi ya Moyo itakayokuwa ya pili nchini, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa matibabu ya kibobezi kwa wagonjwa wa moyo katika Kanda ya Kaskazini.
Ujenzi wa taasisi hiyo unakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 25, ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 20 zimepatikana kupitia michango ya wadau mbalimbali. Kwa sasa, ujenzi umefikia takribani asilimia 35.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chiseo, amesema ujenzi wa taasisi hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 55 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo.
Amesema mradi huo ni moja ya mafanikio makubwa ya KCMC, kwani utawezesha utoaji wa huduma za kibobezi kwa wagonjwa wa moyo katika Kanda ya Kaskazini na maeneo jirani.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, kati ya asilimia 30 hadi 40 ya wagonjwa wa moyo wanaotibiwa nchini wanatoka Kanda ya Kaskazini, hali iliyochochea uamuzi wa kuanzisha kituo hicho ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
“Kwa muda mrefu wagonjwa wa moyo walilazimika kwenda katika Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) kupata matibabu ya kibobezi, lakini sasa tumeona umuhimu wa kuanzisha huduma hiyo hapa Kaskazini,” amesema Chiseo.
Ameeleza kuwa zaidi ya wananchi milioni 11 kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini wanategemea huduma za KCMC, huku hospitali hiyo pia ikihudumia wagonjwa kutoka nchi jirani zikiwemo Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na kusini mwa Kenya.
Amesema wananchi wanaweza kuchangia ujenzi wa taasisi hiyo kupitia mfumo wa TanLink, ambapo kila mwananchi anapewa siku 90 za kuchangia kulingana na uwezo wake.
“Tunahimiza kila mwenye uwezo, hata kidogo, kushiriki kuchangia ili kukamilisha ujenzi wa taasisi hii muhimu kwa afya za Watanzania,” amesema.
Chiseo amesema sambamba na ujenzi huo, hospitali imewekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wake kwa kuwapeleka baadhi yao kusoma nje ya nchi ili kuhakikisha huduma zitakazotolewa zinakuwa na viwango vya kimataifa.
Amesema taasisi hiyo itatoa huduma mbalimbali za kibobezi ikiwemo upasuaji wa moyo, huduma za dharura na matibabu ya kisasa ya magonjwa ya moyo, hatua itakayowezesha Watanzania kupata matibabu ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje.
Katika hatua nyingine, amesema hospitali hiyo imeanza pia kutoa huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani huku ikiendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema wa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Chiseo, kati ya wagonjwa 40 hadi 100 wa saratani hupokelewa hospitalini hapo kila siku, huku takribani wanawake wanne wakifanyiwa upasuaji wa kuondoa matiti kila wiki kutokana na saratani ya matiti.
Amesema changamoto kubwa ni kuwa wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiwa tayari katika hatua za juu za ugonjwa huo.
“Wengi wanakuja katika hatua ya tatu au ya nne ya saratani, lakini tunaendelea kutoa elimu kwa jamii na kuwahamasisha wanawake kujipima wenyewe ili kugundua saratani mapema,” amesema.
Aidha, amesema KCMC inaendelea kufanya tafiti kubaini sababu za kuongezeka kwa saratani, hususan kwa watoto, pamoja na sababu za ongezeko la magonjwa ya moyo katika Kanda ya Kaskazini.
Pia ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo, hususan wagonjwa wa saratani na wanaofanyiwa upasuaji.
Ameongeza kuwa magonjwa mengi ya moyo yanachangiwa na shinikizo la damu pamoja na kisukari, hivyo wananchi wanashauriwa kufuata mtindo bora wa maisha ili kujikinga na magonjwa hayo.
“Tumewekeza pia katika kutoa elimu ya afya kwa jamii ili kusaidia kuzuia magonjwa kabla hayajatokea,” amesema.



