BAGHDAD, Iraq
WIZARA ya Afya ya Iraq imeripoti ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, huku ikitupa lawama kwa raia wa nchi hiyo wanaosafiri kwenda nje ya nchi.
Wiki za hivi karibuni zimeshuhudia maambukizi mapya nane yaliyoripotiwa Kaskazini mwa Jimbo la Duhok na Kusini mwa Dhi Qar. Hiyo inafanya maambukizi kufikia 200.
Taarifa ya Wizara imeeleza kuwa sehemu kubwa ya maambukizi mapya ni ya raia waliorejea Iraq wakitokea ughaibuni walikokwenda kwa masomo, matibabu au shughuli za utalii.
Kwa upande mwingine, Wizara imeeleza kuwa kati ya maambukizi hayo, wapo pia watoto kadhaa wenye umri chini ya miaka 12.
Taarifa zinaeleza kuwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ni zaidi ya 2,000 nchini humo, ingawa hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024.
Dhulfiqar Ahmed, ambaye ni mwanachama wa Chama cha Madaktari nchini Iraq, anasema Serikali inapaswa kuja na mkakati madhubuti wa kudhibiti kasi ya maambukizi mapya.
“Hata hayo yanayoonekana kuwa ni maambukizi machache, hayapaswi kupuuziwa,” anasema na kusisitiza kuwa mamlaka zinapazwa kushirikisha shule na vyuo vikuu katika kampeni za kukabiliana na Ukimwi.


