LONDON, Uingereza
SIKU chache tu baada ya kutangazwa kuwa kocha wa Chelsea, Liam Rosenior amesisitiza juu ya usajili wa kipa mpya.
Akiwa kocha wa Strasbourg ya Ligi Kuu nchini Ufaransa (Ligue 1), kipa wake tegemeo alikuwa ni Mike Penders, ambaye ripoti zinadai kuwa huenda akamvuta Stamford Bridge.
Ifahamike kuwa Penders ni kipa wa Chelsea anayecheza kwa mkopo Strasbourg, klabu ambayo pia inamilikiwa na mabosi wa vigogo hao wa London.
Licha ya kusema Filip Jorgensen na Rob Sanchez ni makipa wazuri, Rosenior amekiri kuwa kikosi chake kinahitaji maboresho katika eneo hilo.
Hata hivyo, ni kwa muda mrefu mabosi wa Chelsea wamekuwa wakimfukuzia kipa wa AC Milan, Mike Maignan.
Blues walijaribu na kukaribia kumsajili wakati wa usajili wa kiangazi mwaka jana lakini dili hilo lilitoa mbawa dakika za mwisho kabla ya dirisha kufungwa.


