Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA wengi, ndoa ni tukio muhimu. Katika baadhi ya imani, ndoa ni hatua ya pili ya maisha ya binadamu baada ya kuzaliwa. Kifo ni hatua ya tatu na ya mwisho.
Hivyo, kutokana na uzito huo, sherehe za ndoa zimekuwa zikigharimu fedha nyingi, ikiwa ni katika kuipa umuhimu hatua hiyo ya pili ya maisha ya binadamu hapa duniani.
Hata hivyo, zipo sherehe za ndoa zilizoacha mshangao mkubwa kutokana na fedha nyingi zilizotumika.
Said Gutseriev, Khadija Uzhakhova
Mwaka 2016, tajiri wa kampuni za mafuta nchini Urusi, Gutseriev, alifunga ndoa na mpenzi wake, Khadija, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu.
Inatajwa kuwa ndiyo ndoa ya Bei mbaya zaidi duniani baada ya kiasi cha Dola bilioni moja kutumika katika sherehe.
Si tu gauni la bi harusi lenye uzito wa kilogramu 25, bali pia sherehe zilishuhudia wanamuziki wakubwa duniani, akiwamo Jeniffer Lopez, wakitumbuiza.
Anant Ambani, Radhika Merchant
Mwaka jana, India iliitikisa dunia kwa ndoa ya bilionea Ambani, ambaye alifunga ndoa na bibiye Radhika.
Sherehe ilidumu kwa wiki moja, hivyo ndoa yao kugharimu kiasi cha Dola milioni 600. Ni sawa au zaidi ya bajeti ya baadhi ya hafla za serikali nchini India.
Charles, Diana
Mwanamfalme wa Uingereza, Charles, alifunga ndoa na Diana mwaka 1981. Wakati huo, ikitajwa kuwa ni ndoa ya karne baada ya kugharimu Dola milioni 140.
Ni ndoa iliyofuatiliwa na watu milioni 750 duniani. Kiasi hicho ni kwa thamani ya sasa, kwamba kwa mwaka 1981 ilikuwa ni Dola milioni 48.
Sheikh Mohammed, Hind
Ndoa ilifungwa mwaka 1979. Mohammed bin Rashid Al Maktoum wa Dubai alipomua Mwanamfalme Hind Maktoum.
Sherehe zilifanyika uwanjani na zilimalizika baada ya wiki moja, huku bajeti ya ndoa nzima ikiwa ni Dola milioni 137.


