3.2 C
New York

Tanzania v Nigeria; Dakika 90 za ‘Daudi na Goliath’ AFCON 2025

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HII ni mechi ya kwanza kwa kila timu msimu huu wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025). Ni mechi ya leo Desemba 23 ya Kundi C, ambapo Nigeria itakwaana na Taifa Stars katika Uwanja wa Complexe Sportif de Fes.

Super Eagles wataingia katika mchezo huo wakiwa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda, ikikumbukwa kuwa walifika fainali msimu uliopita wa AFCON.

Kwa Stars, licha ya kushiriki kwa mara ya nne, watashuka dimbani wakisaka ushindi wao wa kwanza katika historia ya mashindano hayo.

Eagles, si tu wana machungu ya kukosa tiketi ya fainali zijazo za Kombe la Dunia, bali pia wana ukame wa AFCON kwani ni miaka 12 sasa imepita tangu walipotwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Nigeria watashuka dimbani wakiwa nafasi ya 38 katika viwango vya ubora wa soka duniani, ikiwa juu kwa nafasi 74 ukilinganisha na Stars.

Aidha, Stars haijapata ushindi katika mechi saba zilizopita, na badala yake imefungwa nne na kupata sare tatu. Michezo saba imeshuhudia Stars ikifunga mabao mawili pekee.

Katika mechi tatu za hivi karibuni, Stars haijaweza kutikisa nyavu mbele ya Eagles, ikiwamo ile ya mwisho ya kipigo cha bao 1-0.

Kwa mujibu wa historia, hii itakuwa mara ya pili kwa Nigeria na Stars kukutana katika michuano hiyo ya AFCON. Mara ya kwanza ilikuwa wakati wa fainali za mwaka 1980, ambapo Nigeria wakiwa wenyeji walishinda mabao 3-1.

Vikosi

Eagles: Nwabali, Osayi-Samuel, Ajayi, Bassey, Sanusi, Ndidi, Iwobi, Onyeka, Chukwueze, Lookman na Osimhen.

Stars: Suleiman, Kapombe, Mwamnyeto, Job, Hussein ‘Tshabalala’, Miroshi, Feisal, Msuva, M’Mombwa, Allarakhia na Samatta.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img