4.1 C
New York

Miaka 14 bila Muammar Gaddafi; Walibya wamekipata walichokitaka?

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WAKATI wananchi wa Libya walipoingia barabarani katika miji mbalimbali Februari, 2011, kilio chao kikubwa kilikuwa ni uhuru, ambao waliamini wanaukosa chini ya utawala waliouita wa kidikteta wa aliyekuwa Rais wao, Muammar Gaddafi.

Ikiwa ni miaka 14 imepita tangu walipouangusha utawala wa Gaddafi siku hiyo, kama kuna walichokipata Walibya, basi ni majuto, simanzi na hata vilio visivyo na sauti.

Tangu kung’olewa madarakani kwa Gaddafi na kisha kifo chake, Walibya wamekuwa wakiishi maisha ya tabu, nchi hiyo ikigeuzwa masikani ya machafuko yanayotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Libya ambayo katika baadhi ya maeneo yake, vikundi vya kigaidi, ikiwamo ISIS, vimekita mizizi na kugeuza ardhi ya nchi hiyo kuwa makazi yake.

Ni Libya ambayo haijashuhudia Uchaguzi Mkuu tangu mwaka 2014 na sasa maisha yanaenda bila uwepo wa serikali kuu, huku nchi ikiwa imegawanyika vipande viwili. Kwa upande mmoja, ipo Serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu, Abdul Hamid Dbeibah, ambao ndiyo inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na makao makuu yake ni mjini Tripoli.

Lakini pia, Serikali nyingine ni ya Mashariki mwa Mji wa Benghazi na kwa sasa inaongozwa na Waziri Mkuu, Ossama Hammad. Hata hivyo, kile wanachokiona wananchi ni kwamba wanachopigania viongozi wa pande mbili hizo ni masilahi binafsi tu na si kuisaidia Libya.

Wakati huo huo, miaka 14 bila Gaddafi inaishuhudia Libya ikiwa katikati ya mataifa mengine yanayopishana mlangoni kuingia na kujichotea rasilimali zilizopo. Mathalan, kwa sasa wanajeshi wa Uturuki wameweka makazi Magharibi mwa Libya, wakati wale wa Urusi wanapatikana kwa wingi katika maeneo ya Mashariki.

Ni kile alichokikataa Gaddafi mwaka 1970, alipogomea uwepo wa kambi za kijeshi za Marekani na Uingereza katika ardhi ya Libya.

“Mataifa mengine yanataka kuifanya Libya iendelee kukosa utulivu zikitumia wanajeshi kuwatia hofu wananchi ili kuendelea kuiba rasilimali zetu,” anasema mchambuzi wa siasa nchini Libya, Doukali Meghri.
Kama hiyo haitoshi, Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar yanashutumiwa kwa vyombo vyake vya habari kuripoti taarifa zinazolenga kuchochea uadui uliopo kati ya Serikali mbili zinazoiongoza Libya.

Kwa upande wake, Misri na Algeria, licha ya ujirani wao na Libya, hakuna inayojishughulisha na hicho kinachoendelea. Ni kutokana na mazingira magumu hayo, Walibya sasa hawakipati kile walichoamini wanakikosa chini ya utawala wa Gaddafi.

Leo hii, Libya haina tena Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tripoli, ambao uliharibiwa vibaya wakati wa machafuko ya mwaka 2014 kati ya wananchi na vyombo vya dola, yakitajwa kuwa ni makubwa zaidi kuwahi kutokea.

“Unaweza kuona, tulikuwa na uwanja mkubwa wa ndege na kila siku zilikuwepo ndege zilizokuwa zikienda maeneo mbalimbali, ikiwamo Ulaya,” anasema Fouad Fazzani, mtaalamu wa masuala ya utalii nchini Libya.

“Miaka michache kabla ya mapinduzi (ya kumtoa Gaddafi), tulianza kupokea maelfu ya watalii kote nchini. Kwa sasa, sekta hii ya utalii imekwama kutokana na hali ya nchi tangu mwaka 2011.”

Aidha, miradi mingi ya uwekezaji nayo imesimama, ukiwamo ule mkubwa zaidi duniani wa maji uliopachikwa jina la ‘Great Man-Made River’. Ni mradi uliolenga kuimarisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na shughuli za kilimo.

Kutokana na changamoto za aina hiyo, wananchi walio wengi wameanza kuhisi kuwa utawala wa miaka 42 wa Gaddafi ulikuwa bora mno kuliko mateso wanayopitia kwa sasa. Wengi wanakumbuka Gaddafi alipoingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi, akimtoa madarakani Mfalme Idris mwaka 1969.

Watakumbuka alivyobinafsisha viwanda alivyovikuta vikiwa chini ya kampuni za kigeni, ambazo zilikuwa zikishirikiana na Mfalme Idris katika ‘kutafuna’ rasilimali za Walibya.

Watakumbuka namna utawala wa Gaddafi ulivyotumia utajiri wa mafuta wa nchi hiyo kuondosha gharama katika huduma za elimu (hadi chuo kikuu) na afya, pia akilinda ustaarabu wa jamii yake kwa kupiga marufuku unywaji wa pombe na uchezaji wa kamari.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img