4.1 C
New York

Museveni kugombea tena; ni tamaa au uzalendo?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
NI takribani miaka 40 akiwa madarakani na sasa Yoweri Museveni ni miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika mwakani.
Kwamba Rais Museveni haoni sababu ya kukaa pembeni, licha ya uongozi wake wa miongo minne kushindwa kumaliza kero za wananchi, ikiwamo ugumu wa maisha unaotokana na hali mbaya ya uchumi wa Taifa hilo la Afrika Mashariki.
Museveni, ambaye sasa ana umri wa miaka 81, amekuwa rais wa Uganda tangu alipoingia Ikulu mwaka 1986 alipomng’oa kwa mapinduzi ya kijeshi Milton Obote.
Kwa miaka mingi, utawala wake umekumbana na ukosolewaji mkubwa, hasa kwa namna ulivyokithiriwa na vitendo vya rushwa, achilia mbali kudhibiti na kukandamiza haki za binadamu.
Uganda, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, imekuwa ikipoteza euro bilioni 2.4 kila mwaka kutokana na rushwa.
Sarah Bireete, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Center for Constitutional Governance (CCG), amesema Serikali ya Uganda inakabiliwa na kiwango kikubwa cha rushwa.
“Tunapokusanya trilioni 32, basi trilioni 10 hupotea kutokana na rushwa. Hii inaweza kukuonesha hali halisi ya demokrasia hapa Uganda,” anasema.
Takwimu za dunia juu ya masuala ya rushwa, kama zinavyoainishwa na Taasisi ya World Justice Project, zinaonesha kuwa Uganda inashika nafasi ya 126 kati ya mataifa 140.
Wakati huo huo, lipo suala la haki za binadamu, ambapo wakosoaji wa utawala wa Rais Museveni wamejikuta wakiingia matatani mara kwa mara. Wanasiasa wawili wa upinzani, Kizza Besigye na Bobi Wine, ni mfano mzuri.
Kama itakumbukwa, kushikiliwa kwa muda mrefu kwa Besigye kumevuta hisia za jumuhiya za kimataifa na kulaaniwa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu duniani kote.
Wine, mkosoaji mkubwa wa Rais Museveni, anasema: “Ni kwa bahati mbaya sana, ukiukwaji wa sheria ni wa kiwango kikubwa sana nchini Uganda. Siyo polisi, mahakama, wala Bunge; hakuna chombo kinachoweza kuzuia.”
Kwa upande mwingine, ustawi wa haki za binadamu huenda sambamba na uhuru wa kujieleza, ikiwamo vyombo vya habari kupewa uwanja mpana wa kutekeleza majukumu yake.
Isivyo bahati, utawala wa Rais Museveni umeonekana kujenga uadui mkubwa na vyombo vya habari, hali inayotajwa kuzorotesha uhuru wa kujieleza nchini Uganda.
Katika viwango vya ubora wa hali ya vyombo vya habari ya Taasisi ya Waandishi Wasio na Mipaka, Uganda inashika nafasi ya 143 kati ya mataifa 180.
Robert Ssempala, ambaye ni mwanaharakati wa haki za waandishi wa habari, anasema: “Waandishi wengi wanaosakwama (na Serikali) ni wale wanaoripoti taarifa za upinzani.”
Lakini, wakati huo ukiwa ni upande mmoja wa utawala wa Rais Museveni, baadhi ya wananchi wanaamini bado mwanasiasa huyo anafaa kuendelea kuiongoza Uganda kwa miaka mingine ijayo.
“Chini ya Museveni, tumeona maendeleo makubwa ya uhuru wa kisiasa nchini. Ukiwa kama kiongozi wa nchi, lazima uweke mipaka ya vyama vingine vya siasa na kudhibiti namna ya ukosoaji dhidi ya Serikali,” anasema mmoja ya wananchi wanaomuunga mkono Rais Museveni.
Naye Agnes Atim Apea, ambaye pia ni mwananchi anayekubaliana na uamuzi wa Rais Museveni kugombea tena, anasema: “Museveni ameleta mabadiliko mengi katika nchi yetu, kubwa ni amani na utulivu.
Agnes anagusia sekta za kilimo, usafiri na utalii na kusema zimepiga hatua kubwa wakati wa utawala wa Rais Museveni. “Tumeweza kufanya vizuri, hasa katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.”
Hata hivyo, wakati maoni yake yakionesha kuwa Uganda inafanya vizuri kiuchumi, ripoti zinaeleza kuwa bado Taifa hilo linakabiliwa na udhaifu wa kutegemea kwa kiasi kikubwa misaada kutoka nje.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img