4.1 C
New York

Sura mbili tofauti utawala wa Ibrahim Traore

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA upande mmoja, Ibrahim Traore wa Ivory Coast anatajwa kuwa ni shujaa, akionekana kuwa ni mtetezi halisi wa Bara la Afrika mbele ya udhalimu wa mataifa ya Magharibi.
Tujikumbushe; ni miaka mitatu tu imepita tangu Traore alipoongoza mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso na tayari misimamo yake juu ya makaburu inamfanya afananishwe na wanasiasa waliopigania uhuru wa Afrika.
Hata hivyo, upande wa pili wa Traore unakosolewa vikali na baadhi ya wachambuzi na hata taasisi za haki za binadamu. Ni kwa namna anavyoiongoza Burkina Faso tangu alipoingia Ikulu.
Ikumbukwe, alishika madaraka Septemba 30, 2022, baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa Paul-Henri Sandaogo Damiba.
Haijasahaulika kuwa Sandaogo Damiba alihudumu kwa miezi michache tu tangu naye alipoongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomtoa madarakani Rais aliyekuwa amechaguliwa na wananchi, Roch Marc Christian Kabore.
Swali ni je, kwanini Traore anakosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu, wakati anaonekana ni shujaa mbele ya Waafrika walio wengi, hasa huko mitandaoni?
Wakati anaingia madarakani, moja ya ahadi zake kubwa ilikuwa ni kutokomeza vikundi vya kigaidi ndani ya miezi sita tu ya utawala wake.
Achilia mbali ahadi ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Kidemokrasia, ambayo ilizimwa miezi sita tu baada ya kuingia Ikulu, aliposema mchakato huo siyo kipaumbele chake.
Ni mwaka wa tatu sasa, hakuna ahadi iliyotekelezeka na badala yake, Traore anakosolewa kwa kujimilikisha madaraka akitumia nguvu kubwa ya kijeshi.
Traore ameenda mbali zaidi na kufanya mabadiliko makubwa ya sera za nje, ikiwa ni pamoja na kufuta urafiki wa miaka mingi kati ya Burkina Faso na Ufaransa.
Iliwashangaza wengi, ikizingatiwa kuwa Ufaransa imekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na ugaidi nchini Burkina Faso. Mwaka 2023, Traore aliagiza wanajeshi wa Taifa hilo kuondoka nchini mwake.
Na badala yake, aliunganisha nguvu na mataifa jirani ya Mali na Niger, ambayo pia yanaongozwa kijeshi, kuunda muungano wao wa Alliance of Sahel States (AES).
Licha ya pande tatu hizo kuungana na Urusi, bado Traore ni kama amekwama katika kutimiza ahadi yake ya kutokomeza ugaidi nchini Burkina Faso.
Kuthibitisha hilo, ni tukio la Agosti 24, mwaka jana, ambapo waasi walivamia Kaskazini mwa Mji wa Barsalogho na kuua mamia ya raia wasio na hatia.
“Takribani asilimia 70 ya nchi bado iko chini ya utawala wa vikundi vya waasi. Inachofanya Serikali ni kuzuia taarifa zinazoripoti matukio ya aina hii,” anasema mchambuzi wa siasa, Paul Melly.
Aidha, Justin Yarga ambaye ni mwandishi wa habari aliyekimbia Burkina Faso na kuomba hifadhi ya kisiasa nchini Sweden, anasema uongozi wa Traore umekuwa ikitumia mitandao ya kijamii kuficha madhaifu yake.
Ukandamizaji wa haki za binadamu unatajwa kuthibitishwa na hatua ya Traore kupitisha sheria inayopiga vita mapenzi ya jinsia moja, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Burkina Faso kuharamisha vitendo hivyo.
Pia, wanaharakati hawakubaliani na hatua ya utawala wa Traore kuanza kuwafutia uraia wa Burkina Faso wale walioonekana kupaza sautii za kuikosoa Serikali.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za Burkina Faso wanakubaliana kuwa bado uongozi wa Traore unaungwa mkono na wananchi walio wengi, hasa kwa namna anavyoyatunishia msuli mataifa ya Magharibi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img