*Awataka kutumia lugha rahisi ziwafikie walengwa
Na Nadhifa Omary, Morogoro
SERIKALI imewataka wana sayansi nchini na wadau wa afya kufanya tafiti zitakazosaidia kuleta suluhisho juu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya hasa ya unyanyapaa katika jamii.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Grace Maghembe wakati akifunga Kongamano la Kitaifa la Kisayansi lililofanyika katika Hoteli ya Nashera mkoani Morogoro ambapo wadau na wataalamu wa masuala ya sayansi na tafiti walikutana kwa siku mbili kujadiliana kwa pamoja juu ya tafiti mbalimbali walizofanya zenye lengo la kutoa mwelekeo dhidi ya Maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI.
Dk. Maghembe amesema jambo hilo linachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha juhudi za Serikali na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.
“Serikali itaendelea kujivunia wanataaluma wetu hasa wanaofanya tafiti za ndani zitakazoleta suluhisho katika jamii hasa kwenye sekta ya afya, na hakikisheni hizo tafiti mnazofanya zinawekwe kwenye lugha rahisi ambayo kila Mtanzania ataelewa nini kimeandikwa na mzisambaze hadi ngazi ya chini kabisa ya Serikali za Mitaa ili kusudi kila Mtanzania aweze kunufaika na hayo machapisho yenu ya kitaalamu,” amesema Dk. Maghembe.
Aidha, ameipongeza Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa uratibu wa kongamano hilo lililokutanisha wataalam na kujadili masuala muhimu yenye lengo la kutatua changamoto katika sekta ya afya hasa namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.
Pia amepongeza uwepo wa kongamano la vijana na wadau kusaidia uwezeshaji wa makongamano hayo yenye tija kubwa kwa vijana pia ni sehemu muhimu ya kupata maoni yao ili kujua ni namna gani serikali inaweza kuwekeza katika afua zinazowalenga.
“Hivyo, kwa kufanya kongamano la vijana wa vyuo vikuu na hili lililofanyika hapa hoteli ya Nashera kwa siku mbili ambalo limekutanisha wataalamu na wadau mbalimbali wa masuala ya kisayansi katika kujadiliana kwa pamoja juu ya tafiti zilizofanywa zinatoa taswira gani kama taifa kwenye mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI,” amesema Dk. Magembe.
Dk. Maghembe amesema kongamano hili lilikuwa na lengo la kukaa kwa pamoja kwa wadau na kujitathimini ikihusisha serikali na Wadau wa Maendeleo kutekeleza afua mbalimbali lakini pia na kufanya tafiti kwa wakati ili kuona namna ya kutekeleza afua mbalimbali katika kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.
Amongeza kuwa, kupitia kongamano hilo litasaidia serikali kuona kazi zilizofanyika mambo gani yaliyofanyika vizuri na mambo gani ambayo hayakufanyika vizuri na kuonyesha ni yapi ya kujifunza kutoka taasisi mbalimbali.
“Kupitia majadiliano haya yatatuwezesha kuandaa sera itakayotekelezwa kwa jamii kwasababu tayari tumeshafahamu nini jamii inahitaji huko ngazi za chini na kwakuwa tayari tumeshapata taarifa za kitaalamu za kitafiti.
“Lazima tupambane kuhakikisha ifikapo malengo ya 2030, lazima tuangalie tumefikia wapi kwenye jitihada za mapambano kuanzia leo lakini pia kuna changamoto kubwa kuhusiana na changamoto ya kukabiliana maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lazima iende kwa vitendo,” amesema.
Ameongeza kuwa; “Tumepiga hatua kubwa kwenye unyanyapaa lakini bado kuna changamoto kubwa hadi leo watu wanaogopa kujitokeza kujitangaza kuwa ana maambukizi na kuwa hawako huru kuzungumza kwa familia na marafiki na waathirika wanavyokaa kimya ndio kunasababisha kuongezeka kwa maambukizi mapya jambo ambalo linahitaji tafiti za kina kuhusu suluhisho la kupambana na unyanyapaa katika Jamii,” amesema Dk. Magembe.