Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Tanzania ni kati ya nchi chache barani Afrika ambazo zinafanya vema katika kupambana na janga la UKIMWI ambapo Takwimu zinaonyesha kuwa imefanikiwa kushusha maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI(VVU) kutoka asilimia 7.7 mwaka 2003/2004 hadi asiliamia 4.4 mwaka 2022/2023.
Februari 6, 2024 akifungua mkutano wa mapitio ya kimkakati wa PEPFAR COP muhula wa 23 jijini Dar es Salaam, uliolenga kutathmini hatua iliyofikiwa kuhusu mwitikio wa VVU katika udhibiti wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Tanzania imepiga hatua katika nyanja za mwitikio wa UKIMWI.
Waziri Ummy alibainisha kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya UNAIDS 2022, Tanzania imefikia Mkakati wa Kimataifa wa UKIMWI 2021 hadi 2026 kwa lengo la matibabu.
Aidha, Waziri Ummy amesema kupaumbele katika masuala ya VVU/UKIMWI ni pamoja na kulinda mafanikio yaliyofikiwa, kupunguza maambukizi mapya hususan kwa vijana balehe na kupunguza maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Tanzania tumepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za mwitikio wa VVU ambapo kwa mujibu wa ripoti ya UNAIDS 2022, Tanzania imefikia Mkakati wa Kimataifa wa UKIMWI 2021 hadi 2026 kwa lengo la matibabu.
“Mafanikio haya yamechangiwa na matokeo ya Utafiti wa Athari za VVU Tanzania Mwaka 2022-2023 (HII 2022-2023) ambao uliripoti kufikiwa kwa malengo ya UNAIDS 95-95-95 kwa 82.7%, 97.9% na 94.3% (ngazi ya jamii).
“Ikijumuisha 95% ya watu wanaokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU na wanafahamu hali zao za VVU, 95% ya walioambukizwa VVU na wanatumia dawa za kufubaza VVU (ARVs) na 95% ya wale wanaotumia ARVs walifikia hali ya kufubaza VVU,” alisema Ummy.
Juhudi hizo za Tanzania katika kudhibiti janga la UKIMWI zimekuwa zikipewa nguvu na washirika wa Kimataifa wakiwemo PEPFAR, Global Fund, UNAIDS, WHO, UNICEF, CDC, USAID, DOD pamoja na Peace Corps hata ambayo kwa sasa imeilazimu Serikali kusaka vyanzo vyake vya ndani kwa ajili ya kutunisha mfuko wa UKIMWI (Aid Trust Fund-ATF) hatua itakayoisaidia kutekeleza afua za UKIMWI hata pale wafadhili watakaporudi nyuma na kutimiza lengo la kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.