2 C
New York

Simulizi ya Zuhra na mapambano dhidi ya ndoa za utotoni

Published:

Na mwandishi wetu, Zanzibar

WAKATI Zuhra (Si jina lake halisi) alipokuwa na umri wa miaka 17 tu, hatima ya maisha yake ilikuwa tayari imeanza kuamuliwa bila ridhaa yake. Katika jamii yake visiwani Zanzibar, mipango ya kumwozesha ilikuwa imeanza kufanyika. Maisha ya shule yalitarajiwa kuishia hapo, na ndoto zake za utotoni zingeishia mapema.

Kama ilivyo kwa wasichana wengi wanaokabiliwa na ndoa za utotoni, Zuhra hakuwa na uwezo mkubwa wa kupinga uamuzi huo. Hata hivyo, hatua moja ya haraka ilibadili kabisa mkondo wa maisha yake.

Kupitia Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi katika eneo la Madema, Unguja, linaloungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) pamoja na Serikali ya Finland kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zuhra alipata ulinzi, heshima na muhimu zaidi, haki ya kufanya uamuzi kuhusu maisha yake.

Baada ya kesi yake kubainika, watoa huduma waliopata mafunzo walichukua hatua za haraka kuhakikisha anapata ulinzi wa haraka na kufungua kesi rasmi ili kulinda usalama wake na kuhakikisha matakwa yake yanazingatiwa katika maamuzi yote yanayofuata.

Msaada huo haukuishia kwa Zuhra pekee. Wazazi wake walipatiwa ushauri wa kisaikolojia na kushirikishwa katika majadiliano yaliyolenga kubadili mitazamo na mila zinazochochea ndoa za utotoni. Kupitia mchakato huo, familia ilifanya uamuzi mkubwa uliobadili maisha: mpango wa ndoa ulifutwa, mahari ikarudishwa na wazazi wakaahidi kuwapeleka watoto wao wote shule.

Baada ya kuondokana na tishio la kuolewa utotoni, Zuhra alirejea shuleni akiwa na ari mpya ya kusoma. Leo hii, amemaliza elimu yake ya sekondari na anaendelea na masomo ya sheria. Ndoto yake ni kuwasaidia wanawake na wasichana waliokumbwa na ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wengine hawapiti katika hatari kama aliyowahi kukabiliana nayo.

“Nataka kuwasaidia wasichana kuelewa haki zao na kujua kwamba ndoto zao zina thamani,” anasema Zuhra.

Safari ya Zuhra inaakisi matokeo ya programu ya “Chaguo Langu, Haki Yangu”, inayolenga kuimarisha juhudi za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia ushirikiano huu, wanawake na wasichana wengi zaidi, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata huduma zinazomweka manusura mbele pamoja na maeneo salama ambapo sauti, haki na maamuzi yao vinaheshimiwa.

“Mwekezaji bora zaidi kwa jamii ni kumuwezesha msichana kutimiza ndoto zake,” anasema Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania. “Kwa kushirikiana na wadau kama Serikali ya Finland, tunabadilisha ulinzi kuwa fursa na kuhakikisha hakuna msichana anayeachwa nyuma.”

Baba wa Zuhra, Zimbwe Msumi (Si jina lake halisi), anasema tukio hilo limebadilisha kabisa mtazamo wake kuhusu namna ya kumlinda binti yake.

“Kama baba, awali nilidhani namlinda binti yangu kwa kumwozesha mapema. Lakini sasa nimeelewa kwamba ulinzi wa kweli ni kusikiliza ndoto zake na kuhakikisha anaendelea na elimu. Haki ya elimu kwa binti yangu ina thamani kubwa kuliko mila au mahari yoyote,” anasema.

Anaongeza kuwa wazazi kote Tanzania wanapaswa kusimama kutetea haki za mtoto wa kike, kuhakikisha wanabaki shuleni na kuwasaidia kufikia ndoto zao. “Tunapowalinda wasichana wetu, tunalinda mustakabali wa taifa letu,” anasema.

Katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, simulizi la Zuhra linatukumbusha kwamba pale wasichana wanapopewa nafasi ya kutetea haki zao na kufanya maamuzi kuhusu maisha yao, jamii nzima husogea karibu zaidi na usawa na haki.

Kupitia ushirikiano unaowekeza katika heshima, elimu na fursa, wasichana wengi zaidi kama Zuhra wanaweza kubadilisha hatima zao na kusaidia kujenga dunia ambayo wanawake na wasichana wote wanafurahia haki, usawa na uwezeshaji.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img