DAKAR, Senegal
Bunge la Kitaifa la Senegal limepitisha kwa wingi muswada unaoongeza adhabu kwa watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, hatua inayotarajiwa kuimarisha sheria zilizokuwepo awali dhidi ya vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa za wabunge, muswada huo ulipitishwa Jumatano kwa kura 135 huku wabunge watatu wakikosa kushiriki katika upigaji kura. Sheria hiyo inapendekeza kuongeza adhabu ya kifungo hadi miaka 10 jela kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kushiriki vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, pamoja na kuharamisha juhudi zozote za kuhamasisha au kuendeleza mahusiano ya aina hiyo.
Hatua hiyo inatekeleza moja ya ahadi kuu za kampeni za serikali iliyoingia madarakani mwaka 2024 chini ya uongozi wa Rais Bassirou Diomaye Faye na Waziri Mkuu Ousmane Sonko, ambao walisisitiza kulinda maadili ya kijamii na kitamaduni ya nchi hiyo.
Baada ya kupitishwa na Bunge, muswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na Rais Faye ili kuanza kutumika rasmi kama sheria ya nchi.
Senegal tayari ina sheria zinazokataza mahusiano ya jinsia moja, lakini mabadiliko haya yanaongeza ukali wa adhabu na kupanua wigo wa vitendo vinavyoweza kuadhibiwa chini ya sheria hiyo.
Hatua hiyo imeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya haki za binadamu, huku baadhi ya makundi ya kijamii yakisema inalenga kulinda maadili ya jamii, wakati wengine wakieleza wasiwasi kuhusu athari zake kwa uhuru wa kiraia.


