MANCHESTER, Uingereza
KLABU ya Manchester City imeanza mazungumzo ya kumsajili kiungo wa Bayern Munich, Aleksandar Pavlovic.
Nyota huyo ana umri wa miaka 21 na ameshacheza mechi 87 tangu alipojiunga na ‘academy’ ya klabu hiyo ya mjini Munich.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany, amemgeuza Pavlovic kuwa mchezaji tegemeo, ambapo amempa nafasi ya kuanza kikosini katika mechi 25 msimu huu.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ameingia ‘first eleven’ katika mechi zote nane na anatarajiwa kuwa kikosini Jumanne ya wiki ijayo kuikabili Atalanta.
Mtandao wa Caught Offside umeripoti kuwa Man City inamtolea macho staa huyo na imepanga kumsajili majira ya kiangazi, mwaka huu.
Taarifa zinaeleza zaidi kuwa matajiri hao wameshaanza kuwasiliana na watu wa karibu wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani.
Wakati huo huo, Chelsea nayo inatajwa kuitaka saini yake na inatarajiwa kuanza mazungumzo na Bayern hivi karibuni.


