RIO, Brazil
MSHAMBULIAJI huyo wa zamani wa Manchester United na West Ham za England, Jesse Lingard, ametua Ligi Kuu ya Brazil baada ya kusajiliwa na klabu ya Corinthians.
Lingard (33), amejiunga na Corinthians akiwa mchezaji huru aliyemaliza mkataba wake na Seoul ya Ligi Kuu ya Korea Kusini.
Corinthians inafahamika kwa historia yake ya kusajili mastaa waliowika Ulaya, kama ilivyowahi kufanya kwa Socrates, Rivaldo, Carlos Tevez, Ronaldo wa Brazil, na Memphis Depay.
Muingereza huyo amesaini mkataba utakaoisha mwishoni mwa mwaka 2027 na una kipengele cha kuongezewa endapo atafanya vizuri.
Kabla ya kuhamia Brazil, Lingard alipokea ofa nyingi lakini alishawishika kwenda Corinthians baada ya mazungumzo yake na Depay aliyeko klabuni hapo.
Nyota huyo wa eneo la kiungo mwenye umri wa miaka 33 anakuwa mchezaji wa kwanza raia wa Uingereza kucheza Ligi Kuu ya Brazil.
Hata hivyo, ni lazima Lingard afahamu kuwa anakutana na mashabiki wa Corinthians, ambao wana sura mbili.
Ni mashabiki wenye mapenzi makubwa kwa timu yao. Walipoifunga Chelsea mabao 2-1 mwaka 2012, mashabiki 40,000 walisafiri kutoka Brazil hadi Japan kutazama mchezo huo.
Kama hiyo haitoshi, mashabiki hao walianzisha harambee iliyosaidia kupatikana kwa Pauni milioni 6 za kugharamia ujenzi wa uwanja.
Kwa upande mwingine, ni mashabiki wanaosifika kwa ukorofi, hasa pale wanapoona mambo hayaendi sawa kwenye timu hiyo.
Mathalan, maandamano yao ya kupinga viwango vya Roberto Carlos, Tevez, Ronaldo na Javier Mascherano yalisababisha mastaa hao kuondoka klabuni hapo.
Mwaka 2025, mashabiki walivamia makao makuu ya klabu na kufunga mageti wakishinikiza uongozi kujiuzulu.
Rais wa klabu aliondolewa, kabla ya jaribio lake la kutaka kurudi madarakani kwa nguvu. Baadaye, alifunguliwa mashitaka ya rushwa na utakatishaji fedha.
Kwa sasa, Lingard anaikuta Corinthians ikiwa si timu tishio, na badala yake Flamengo na Palmeiras ndizo zinazotawala Brazil na Amerika ya Kusini kwa ujumla.


