LONDON, Uingereza
UNAMKUMBUKA beki wa kati wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil ‘Selecao’, David Luiz? Kwa sasa, nyota huyo ana umri wa miaka 38.
Kwa miaka 20 ya kucheza soka la kulipwa, Luiz amezunguka katika mataifa matano na sasa yuko zake Cyprus akiwa na klabu ya Pifos ya Ligi Kuu nchini humo.
Mlinzi huyo alijiunga na miamba hiyo Agosti, 2025, na kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Fortaleza ya Brazil. Luiz alirejea Ulaya baada ya miaka minne ya kucheza soka nchini kwao.
Katika msimu wake wa kwanza akiwa Pafos, Luiz amecheza mechi 20, zikiwamo sita za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amemaliza dakika 90 za mechi zote nne zilizopita.
Baada ya kucheza Chelsea, PSG na Arsenal, ambapo alitwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa na Ligi Kuu ya England, kwa wa sasa Luiz anafurahia utajiri wake wa Pauni milioni 14.8 akiwa Cyprus.
“Nafurahi sana kuwa hapa. Hakuna aliyetarajia kuwa tungecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu lakini tumefanikiwa kutokana na kazi kubwa tuliyofanya,” anasema Luiz.
“Klabu hii imefanya kazi kubwa kwa miaka mingi. Kocha, wafanyakazi na wachezaji wamekuwa wakipambana kila siku.”
Hata hivyo, bado kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa Chelsea mwaka 2012 imebaki kuwa kumbukumbu nzuri na isiyofutika kichwani kwa Luiz.
“Kwangu, ulikuwa ni usiku wa kipekee, si tu kwa sababu tulitwaa ubingwa, bali pia kwa sabu hakuna aliyetarajia sisi kufika fainali.
“Nafikiri kwa mwaka ule kila mtu alitarajia kuona fainali ikiwa ni kati ya Barcelona na Real Madrid lakini tuliifunga Barcelona na Madrid ikaifunga Madrid.
“Sikutakiwa kucheza fainali kutokana na majeraha lakini ni wachache waliojua kuwa niliingia uwanjani kucheza, tena kwa dakika 120 na kufunga penalti nikiwa na majeraha …”


