Na Wakili Baraka Asajile Gwakabale
MAUAJI yanafafanuliwa kisheria, si kwa maoni ya jamii, na kifungu husika ni cha 196. ‘Murder’ hutokea pale mtu anaposababisha kifo cha mwingine kwa nia ovu (malice aforethought). Bila nia hiyo, kosa halisimami kama murder hata kama mtu amekufa.
Hapa ndipo wengi hukosea. Kifo cha mtu, kwa macho ya jamii, kinaweza kuonekana moja kwa moja kuwa mauaji. Kisheria, hilo halitoshi.
Sheria haishughulikii kilichotokea tu, bali akili ya mtuhumiwa wakati tukio linatokea. Ndiyo maana kifungu cha 196 hakisimami kwenye kifo pekee, kinasimamia nia ovu (malice aforethought).
Nia ovu ina maana gani kwa vitendo? Inamaanisha kwamba upande wa mashtaka lazima uthibitishe kuwa mtuhumiwa: alikusudia kuua, alikusudia kusababisha madhara makubwa yanayoweza kuua au alifanya kitendo cha hatari akijua wazi kuwa kifo ni matokeo ya kawaida ya kitendo hicho.
Bila kuthibitisha hali hiyo ya akili, kesi haiwezi kusimama kama murder hata kama mtu amefariki. Ndiyo maana kuna kesi nyingi ambapo jamii inasema ni mauaji, lakini mahakama inaishia kwenye manslaughter au hata kuachiwa kabisa.
Hapa kuna tofauti ya msingi kati ya hukumu ya kisheria na hukumu ya maoni ya watu. Sheria haifanyi kazi kwa hasira, huzuni, au presha ya umma. Inafanya kazi kwa vigezo vilivyoandikwa.
Muhimu ni kuwa katika murder, kifo ni matokeo. Nia ndiyo kosa. Bila nia, hakuna murder. Nia ovu ndiyo moyo wa kosa.
Kifungu cha 200, Sheria inaeleza wazi maana ya malice aforethought. Inajumuisha nia ya kuua, nia ya kusababisha madhara makubwa, au kitendo cha hatari kinachojulikana wazi kuwa kitasababisha kifo.
Sheria haitafuti tu kilichofanyika, inachambua hali ya akili ya mtuhumiwa kabla na wakati wa tukio. Kifungu cha 200 kinaweka wazi maana ya malice aforethought na kinatoa mwongozo wa moja kwa moja kwa mahakama.
Nia ovu kisheria inaweza kuthibitishwa kwa mambo yafuatayo;
Nia ya kuua moja kwa moja. Hii ni pale mtu anapochukua hatua kwa lengo la wazi la kumaliza uhai wa mwingine.
Nia ya kusababisha madhara makubwa ya mwili yanayojulikana kwa kawaida kusababisha kifo, hata kama mtuhumiwa hakusema alitaka mtu afe.
Maarifa ya hatari. Mtu anapofanya kitendo cha hatari akijua kuwa kifo au madhara makubwa ni matokeo ya kawaida, sheria huchukulia nia hiyo kuwa nia ovu.
Muhimu zaidi, kifungu hiki kinafundisha kuwa Sheria haikubali kisingizio cha “sikutegemea afe” pale hatari inapokuwa dhahiri.
Na badala yake, Mahakama hutazama aina ya silaha au njia iliyotumika, sehemu ya mwili iliyolengwa, nguvu iliyotumika na mwenendo wa mtuhumiwa kabla na baada ya tukio.
Hivi vyote hutumika kusoma akili ya mtuhumiwa bila yeye kusema neno moja. Nia haisomwi kwa maneno, inasomwa kwa vitendo.
Katika murder, kifungu cha 200 ndicho kinachobeba mzigo wa ushahidi. Ukithibitisha nia ovu, kesi inasimama. Ukishindwa, murder huanguka.
Hivyo, kifo peke yake hakitoshi kuthibitisha murder. Vifungu husika ni vya 196 na 203. Mahakama lazima ithibitishe kuwa kifo kilitokana moja kwa moja na kitendo cha mshtakiwa. Mlolongo wa sababu ni lazima uwe wazi.
Kifo pekee hakitoshi, lazima kiunganishwe kisheria na kitendo. Vifungu husika: vifungu vya 196 na 203 vya Penal Code, Cap 16
Hapa ndipo kesi nyingi za murder huanguka. Jamii huona mtu amekufa. Sheria huuliza swali tofauti kabisa: nani, kwa kitendo gani, na kwa mfululizo upi wa sababu?
Itaendelea…Mawasiliano: – 0784745645


