2.9 C
New York

HaloPesa yawagusa watoto yatima msimu wa sikukuu

Published:

Na Iman Nathaniel, Gazetini

KAMPUNI ya Halotel kupitia kitengo cha HaloPesa imefanya ziara katika kituo cha watoto yatima cha Maunga Orphanage Centre, kilichopo Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na kutoa msaada wa vitu mbalimbali.

Ziara hiyo imefanyika leo Desemba 24,2025, ambapo miongoni mwa mahitaji walitoa kituoni hapo ni mavazi, chakula, vifaa vya shule, magodoro, pamoja na vifaa vya afya kama taulo za kike.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo, Meneja Masoko wa HaloPesa, Aidat Lwiza amesema msaada huo ulilenga kuboresha ustawi wa watoto na kusaidia kukidhi mahitaji ya kila siku ya kituo hicho.

Aliwahimiza watoto kuendelea kuthamini upendo, mshikamano na elimu, akisisitiza kuwa elimu ni msingi muhimu wa kujenga maisha bora na mustakabali mzuri wa baadaye.

“Watoto hawa ni hazina ya taifa letu. Kupitia upendo, mshikamano na elimu, tunaamini wanaweza kutimiza ndoto zao na kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii. HaloPesa itaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii zinazogusa maisha ya watu,” amesema Aidat.

Kwa upande wake, Katibu wa Kituo cha Maunga , Issa Ally, aliishukuru HaloPesa kwa moyo wa kujitolea na upendo waliouonesha kwa watoto hao, akibainisha kuwa msaada huo umeleta faraja kubwa na matumaini mapya kwa watoto pamoja na uongozi wa kituo hicho.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa HaloPesa kwa kutukumbuka msimu huu wa sikukuu na kuonesha upendo wa kweli kwa watoto wetu. Msaada huu una mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya watoto waliopo hapa,” amesema Ally.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img