2.9 C
New York

Wizara ya Madini yafuta leseni 73 za uchimbaji na utafiti

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amefuta leseni 73 za utafiti na uchimbaji wa kati baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa yaliyobainishwa na Tume ya Madini.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Novemba 25,2025, jijini Dodoma, Waziri Mavunde amesema mara baada ya kubaini mapungufu kwa wamiliki wa leseni hizo, Tume ya Madini iliwatafuta na kuwaelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa, lakini wameshindwa kutekeleza maelekezo hayo.

“Wamiliki wa leseni za utafutaji madini 44 wameshindwa kurekebisha makosa yao, na vilevile wamiliki wa leseni 29 za uchimbaji wa kati wameshindwa kurekebisha makosa yao,” amesema Waziri Mavunde.

Ametoa wito kwa makampuni yote yaliyopewa leseni kuzingatia masharti na vigezo vya leseni husika badala ya kuzihodhi na kuwanyima fursa wengine, jambo ambalo hatalivumilia.

“Kuna watu wanakuja kuchukua leseni halafu wanahodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi, hawalipi hata kodi na hawatoi ajira, huku baadhi ya leseni zikionyesha zilitolewa tangu 2013 lakini bado wanazo na hawaanzishi shughuli za uchimbaji madini ila wanajiita ni wachimbaji wakati siyo kweli, hao ndio nimeagiza wafutiwa.

“Sitawavumilia watu wanaochukua leseni na kukaa nazo bila kuziendeleza,” amesisitiza Mavunde na kuielekeza Tume ya Madini kusimamia sheria kikamilifu, kuchukua hatua dhidi ya wakiukaji na kufuta leseni zisizoendelezwa bila upendeleo wala kumwonea mtu.

Leseni zilizofutwa ni miongoni mwa 205 ambazo wamiliki wake waliandikiwa hati za makosa na kutakiwa kujibu kwa kuyarekebisha na kuanza uendelezaji., lakini wengine hawakujibu hali inayoonyesha wameshindwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img