2.9 C
New York

Waziri Mkuu aagiza mkandarasi akamatwe

Published:

Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, ameliagiza Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuhakikisha wanamkamata na kuzuia hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi cha Pamoja kilichopo Muhalala, mkoani Singida.

Dk. Mwigulu amesema kuwa mkandarasi huyo aliaminiwa na Serikali kwa kupewa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati uliosimama kwa zaidi ya miaka nane tangu mwaka 2016 ulipaswa kukamilika mwaka 2018.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa Novemba 21, 2025 wakati alipokagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida ambapo atakagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Amesema kuwa jitihada zimefanyika za kuona mradi huo unaendelea lakini mkandarasi amekuwa akileta ugumu katika utekelezaji.“Mkandarasi huyu alitangazwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi na alielekezwa ailipe fidia Tanzania kwa sababu ameicheleweshea mradi.

“Naelekeza, Kamishna wa Uhamiaji kamata hati yake ya kusafiria, asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe, hii ni hujuma ya waziwazi, hii ni dharau ya waziwazi anaifanyia nchi yetu, Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo, tumemuajiri, tunamlipa lakini anajiamulia kama aendelee na kazi au asiendelee, huyu ni mhalifu akamatwe mpaka jambo hili liishe,” amesisitiza Dk. Mwigulu.

Amewataka  wakandarasi wa nje kufahamu kuwa wanapokuja kufanya kazi hapa nchini, watambue Tanzania imewaajiri na wasijione kama wao ni mabosi.

“Ninaelekeza wale washirika wetu katika mradi huu, ndani ya mwezi huu jambo hili liwe limekwisha watuambie wanaendelea ama hawaendelei, na kama hawataendelea Waziri wa Ujenzi uwapatie wakandarasi wadogo wamalizie kazi hii, hii nchi ni yetu na tunawajibu wa kuilinda, na Mheshimiwa Rais Dk. Samia ametuambia hatuna mjomba, tuna mama tu anaitwa Tanzania,”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img