3.6 C
New York

Serikali kuunda Tume kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Rais Samia Suluhu Hassan amesema amehuzunishwa na vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kusema kuwa Serikali imeunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea ili kujua kiini cha tatizo.

Pia amevielekeza vyombo vya sheria vikiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP), kufanya tathimini ya makosa yaliyofanywa na vijana katika vurugu za Oktoba 29, 2025 na kuwafutia makosa wale wote watakaobainika kuwa walifuata mikumbo bila kujua wanachokifanya.

“Ukiangalia clip zile za maandamano unaona kabisa kuna Vijana waliingia kwa kufuta mkumbo, wanaimba kwa ushabiki, naelekeza Ofisi ya DPP kuchuja viwango vya makosa na kwa waliofuata mkumbo wawaachie waende kwa Wazazi wao,”

Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Novemba 14, 2025, Bungeni jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 la Tanzania akikiri kutambua kuwa vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakuwa wakijua wanachokifanya.

 Kabla ya kuzungumza hayo, alianza kwa kuwaongoza Wabunge wa Bunge la Tanzania na wageni waalikwa kusimama na kuomba kwa dakika moja kwa ajili ya wananchi waliopoteza maisha kwenye vurugu na ghasia hizo.

Ametoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, huku pia akiwaomba waliopoteza mali zao kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

 “Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea ili tujue kiini cha tatizo, taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani,” amesema Rais Samia.

Aidha ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa taifa halijengwi kwa ushabiki wa ghasia bali kwa umoja, maelewano na uwajibikaji.

Amewataka kuzingatia misingi ya amani ambayo taifa limejengwa juu yake, akiwakumbusha kuwa matendo ya hasira na fujo yanaweza kuvuruga misingi hiyo. Aidha amewahimiza vijana kutokubali kuchochewa au kushawishiwa kuharibu taifa lao.

Akitoa hotuba hiyo, Rais Samia pia amesema Serikali imedhamiria kuanzisha Wizara itakayoshughulikia masuala ya vijana na anatarajia kuwa na washauri katika Ofisi ya Rais watakaomshauri kuhusu mambo ya vijana ikiwemo changamoto zao.

Mchakato wa Marekebisho ya Katiba kuanza

Katika hatua nyingine amesema ameanza kufanyia kazi suala la marekebisho ya Katiba na ndani ya siku 100 za muhula wa pili wa awamu ya sita  ataanza na  Tume ya usuluhishi na maelewano ambayo itaenda katika hatua ya marekebiisho ya Katiba.

“Hapana shaka kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia ila neno demokrasia kamili linaweza kutafsiriwa kwenye mitazamo tofauti kwani haina kanuni moja.

Kama Taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha, hivyo basi sote kwa umoja wetu tunapaswa tutumie fursa hii kuendelea kujifunza, tukirekebishe na tukubaliane jinsi ya kuendesha ncho yetu kidemokrasia kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi zetu na sio za kuletewa.”Kama tulivyoagizwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi moja ya hatua itakayotufikisha kwenye maelewano hayo ni marekebisho ya Katiba yetu,”

Ataka Watendaji wa Serikali wabadilike

 Kuhusu utendaji wa Serikali, amesema aliahidi wananchi kuwa ataunda Serikali itakayowajibika na kuendelea na mageuzi ya Sera zinazogusa maslahi ya wananchi, hivyo ni lazima viongozi wa ngazi zote za Serikali kubadilika na wasipobadilika kuendana na matarajio basi  watawabadilikia

“Kwa watendaji waliopo Serikalini na wale nitakaowateua wajiande kisaikolojia wajipange vema kukamilisha malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananchi, wananchi wanahitaji mabadiliko chanya na maendeleo, watendaji msipobadilika kuendana na matarajio ya wananchi tutawabadilikia” amesema Rais Samia.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img