20.8 C
New York

Bilioni 23 kuboresha miundombinu hifadhi za Taifa

Published:

Na Mwandishi Wetu

Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) imetenga fedha kiasi cha Sh 23.18 bilioni  kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 2,381.7 na vivuko 69 katika hifadhi za Taifa.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alipokuwa anajibu swali la  Esther Malleko aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji wa Watalii kwenye maeneo ya Hifadhi.

Aidha  Kitandula aliongeza kuwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa watalii itaendelea kuboreshwa kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa hapa nchini, kwa kutumia mikakati ya muda mfupi na ya muda mrefu ili kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inapitika wakati wote wa mwaka. Miundombinu hii ni pamoja na barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Kitandula amesema kuwa Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya KfW imekubali kutoa kiasi cha Euro 500,000 ili kugharamia usanifu na upembuzi yakinifu kwa barabara yenye matumizi makubwa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti inayounganisha Golini – Lango la Naabi – Seronera yenye urefu wa kilomita 68.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img