Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 mwaka 2025 ambapo kwa sasa kima cha chini kitapanda kutoka 370,000 hadi 500,000.
Amesema hayo leo Alhamisi Mei 1,2025 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yaliyofanyuka Kitaifa mkoani Singida.
Rais Samia amesema wafanyakazi wamekuwa na mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi na ataendelea kuboresha maslahi ya watumishi hao.

“Sasa kwa kuwa mcheza kwao hutunzwa, mimi na wenzangu baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda na umepanda kwa sababu ya nguvu zenu wafanyakazi, ninayo furaha ya kuwatangazia kwamba mwaka huu Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa 35.1%, amesema.
Ameeleza kuwa ngazi nyingine za mshahara nazo zitapanda kwa kiwango kizuri jinsi bajeti inavyoruhusu, huku akisema bodi inaendelea kufanya mapitio ili kuboresha viwango vya chini vya mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.