1.6 C
New York

Juhudi za pamoja zinahitajika kudhibiti biashara haramu ya viumbe pori

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Takwimu zinaonyesha kuwa biashara haramu ya viumbe pori inashika nafasi ya nne katika kundi la biashara haramu duniani ikitangaliwa na ile ya dawa za kulevya, Usafirishaji wa bidhaa bandia na Usafirishaji haramu wa binadamu.

Hii ni sawa na kusema kwamba biashara haramu haiathiri tu Tanzania bali ni Dunia nzima, huku ikiwa na athari mbalimbali katika nyanja za kiuchumi, kijamii na namna nyingine.

Kiongozi wa Sera ya Usimamizi wa Maliasili kutoka katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili Activity(TMA), Allen Mgaza akifafanua jambo wakati wa warsha hiyo iliyofanyika hivi karibuni mjini Bagamoyo.

Allen Mgaza ni Kiongozi wa Sera ya Usimamizi wa Maliasili kutoka katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili Activity(TMA) akizungumza juzi mjini Bagamoyo katika Warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa USAID kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Amesema biashara ya viumbe pori imekuwa ikifanyika kwa siri sana na mtandao wake ni mkubwa unaohusisha watu wenye nguvu kubwa ya kifedha.

“Biashara haramu ya viumbe pori ni tatizo kubwa sana na inashika nafasi ya nne duniani katika biashara haramu na katika hili ni lazima kuwe na juhudi za pamoja za kimataifa, nchi kushirikiana, wizara na taasisi tofauti kufanya kazi kwa pamoja katika kupambana na biashara hii haramu ya viumbe pori.

“Hii inatokana  na kwamba ni biashara inayofanyika kwa siri kubwa sababu ni haramu na watu wanaofanya hizi biashara wanasafirisha kwa siri na mbinu mbalimbali ili kupunguza mwanya wa kukamatwa na mamlaka, hivyo ikishakuwa hivyo lazima nguvu iwe kubwa katika kuhakikisha kuwa aina hii ya biashara inadhibitiwa,” amesema Mgaza.

Katika hatua nyingine, Mgaza ametoa wito kwa waandishi wa habari kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kusaidia jamii kubainia madhara ya biashara hii.

“Ni muhimu kutoa elimu kwa jamii kwamba madhara ya mtu kujihusisha na biashara hii ikiwamo kuwezesha makundi yaliyo katika mtandao huu basi umeliangusha taifa lako kwania biashara hii ikifanyika kiharamu utakuwa umeliangusha taifa lako sababu ikifanyika hivyo tunapoteza pato na tunapoteza hawa viumbe.

“Sababu kwa miaka mingi viumbe vinavyowindwa kiharamu mwisho wa siku vitapotea, sitamani ifike kipindi watoto wetu au wajukuu tuwaonyeshe picha za wanyama badala yake waje waone na kufurahia rasilimali hizi za wanyamapori ambazo kama nchi tumebahatika kuwa nazo,” amesema.

Viumbe vinavyofanyiwa biashara haramu

Mgaza ametaja baadhi ya viumbe pori ambavyo vinafanyiwa biashara haramu kuwa ni pamoja na mimea ya pori ikiwamo msandari ambao watu wanauchukua na kukata vipande vyake bila kufuata sheria.

“Mbali na mimea kuna mnyama anaitwa Kakakuona ambaye magamba yake yamekuwa yakisafirishwa mara kwa mara, mfano kuna kesi ilitokea Malaysia ambapo kuna tani sita za magamba ya kakakuona zilikamatwa, hivyo tukifikiria umbo la kakakuona hadi upote magamba ya kiwango hicho maana yake ni wanyama wengi wameuwawa, hivyo biashara hii ikifanyika kwa miaka minne mpaka mitano basi wanyama hawa watapotea,” amesema Mgaza.

Juhudi za udhibiti zimefikia wapi

Mgaza anasema kuwa kama wadau wanafurahi kuona kwamba nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania zimesaini mkataba wa Vyama vya Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Viumbe vilivyo Hatarini Kutoweka (CITIES) ambao ni mkataba wa kimataifa unaodhibiti biashara ya kimataifa ya viumbe pori vilivyohatarini kutoweka.

“Tumerekebisha sheria yetu kwa kuweka sheria ambayo inaakisi mikataba ya kimataifa iliyokubaliana, tunasheria nzuri sana katika hili, hivyo nadhani kutoa elimu ni muhimu lakini usimamizi wa sheria ni jambo jingine.

“Kwanza kunahitajika uwezeshwaji kwa vyombo vyetu vinavyosimamia viumbe pori hawa wakiwamo TAWA(Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania) na vingine,” amesema Mgaza.

Takwimu zikoje

Ripoti hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa Ofisi ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) ya mwaka 2020 iliyopewa jina la “Uhalifu wa Wanyama pori duniani ya mwaka 2020” inabainisha kuwa, Ghada Waly amesema “Mitandao ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa inajipatia faida kutokana na biashara haramu ya wanyama pori, lakini watu masikini ndio wanaolipa gharama ya uhalifu huo,”.

Kakakuona ndio waosafirshwa zaidi kiharamu

Ripoti inasema kati ya mwaka 2014 na 2018 kulikuwa na ongezeko kubwa la mara 10 la ukamatwaji wa magamba ya kakakuona yaliyokuwa yakisafirishwa kiharamu na hivyo kufanya wanyama hao kuwa ndio wanyama pori wanaosafirishwa zaidi kiharamu duniani.

Pia imesema karibu aina 6,000 za viumbe vilikamatwa katika muongo uliopita vikisafirishwa kiharamu wakiwemo wanyama, lakini pia mijusi, matumbawe, ndege na samaki.

Ripoti hata hivyo haikutaja nchi yoyote kuwa ndio chanzo cha zaidi ya asilimia 9 ya idadi yote ya wanayana na mimea iliyokamatwa ikisafirishwa kiharamu, huku washukiwa wa usafirishaji huo haramu wakiwasilisha takribani watu kutoka mataifa 150 na hivyo kudhihirisha kwamba asili ya uhalifu huu ni duniani kote.

Usafirishaji haramu wa mbao waongezeka

Ripoti hiyo pia imeilinisha na kutathimini masoko ya usafirishaji haramu wa mbao, pembe za ndovu, pembe za vifaru, magamba ya kakakuona, jamii ya mijusi, paka shume na aina ya samaki kutoka Ulaya wanaofanana na nyoka.

Ripoti inasema mwenendo unaonyesha kwamba mahitaji ya pembe za ndovu na za vifaru kutoka Afrika yanapungua ikimaanisha kwamba masoko ya bidhaa hizo ni madogo kuliko ilivyopendekezwa hapo awali.  

Ripoti inakadiria kwamba bidhaa hizi mbili zilitengeneza zaidi ya dola milioni 600 kila mwaka kati ya mwaka 2016 na 2018 huku kwa mwaka 2023 kiwango hicho kikipaa na kufikia dola bilioni 23.

Wakati huohuo mahitaji ya bidhaa za mbao yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika miongo miwili iliyopita.

Na biashara haramu ya mbao kutoka Afrika imeingia kwenye mnyororo halali kwa ajili ya biashara ya samani. 

Pia ukamatwaji wa bidhaa za chui umeongezeka lakini wasafirishaji haramu wanania ya bidhaa za aina nyingine ya paka wakubwa ili watumike kama mbadala wa chui.

Mbali ya aina iliyozoeleka ya biashara sasa biashara hiyo imeingia katika njia ya kidijitali na wasafirishaji haramu wamekuwa wakiuza mtandaoni na kupitia program tumishi mbalimbali wanyama walio hai na jamii ya mijusi kama nyoka na pia mifupa ya chui miongoni mwa vitu vingine.

JET

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amebainisha kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.

Mradi wa Tuhifadhi Maliasili ni wa miaka mitano na unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyama na viumbe hai nchini Tanzania.

“Kupitia mafunzo haya, waandishi wa habari wanapata maarifa, ujuzi na  mtazamo chanya wa kuripoti taarifa za uchunguzi kuhusu uhifadhi wa viumbe hai na mabadiliko ya tabianchi kwa usahihi zaidi.

“Hivyo, JET kwa kushirikiana na wadau wengine jukumu letu ni kuwajengea uwezo wanahabari katika eneo la uhifadhi ili kujua namna ya kuchunguza, kuripoti juu viumbe hivi vilivyohatarini kutoweka ikiwamo biashara hii haramu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img