21 C
New York

Makala| Vipepeo; kitega uchumi kinachokumbukwa Muheza

Published:

*Serikali yasisitiza wananchi kuwa na subira

Na Faraja Masinde, Muheza

“…tuliumia sana, tukawaachia tu wakaruka na kwenda zao. Tukasema hatuna cha kufanya… na wakati huo ndiyo vipepeo walikuwa wameongezeka kuliko wakati mwingine wowote ule,” Jestina Bakari.

Ni majira ya saa 9 na dakika 6 ikiwa na sekunde zake 57 Alasiri ndani kitongoji cha Kagera, Kijiji cha Antakae, Kata ya Kwezitu inayopatikana katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Misitu ya Amani Nilo wilayani Muheza mkoani Tanga, Kaskazini Mashariki mwa Tanzania nikiwa sambamba na wenzangu ambao ni Wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) katika kutekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

Tulifunga safari kutembelea kitongoji hiki cha Kagera ndani ya kijiji cha Antakae kwa ajili ya kuangalia hali ilivyo baada ya tangazo la Serikali la Machi 17, 2016 kupiga marufuku usafirishwaji wa wanyama pori hai nje ya nchi ambapo liligusa pia vipepeo.

Kwani Kata ya Kwezitu ni miongoni mwa zilizosifika kwa kufanya vizuri katika biashara hii ya vipepeo kupitia mradi wa Amani Bautterfly Project uliokuwaukisimamiwa na Shirika la Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFCG).

Ni wazi kuwa kwa sehemu kubwa mradi huo ulisaidia wananchi kujiletea maendeleo kwa haraka huku wakitunza mazingira.

Hata hivyo, kwasasa ni kama hakukuwahi kabisa kuwa na mradi huo, kwani hata miundombinu iliyotumika kwa ajili ya kufugia vipepeo hao tayari imeharibika na hata sehemu nyingine kusahaulika kabisa, lakini kinachobaki katika akili ya wananchi hao ni mafanikio yanayoonekana kwa macho ambayo yalichochewa na mradi huo.

Hauhitaji ushahidi zaidi kuamini kuwa mradi huo ulikuwa ni kila kitu kwa wananchi hawa kulingana na namna kila mmoja kwa wakati wake anavyouzungumzia kwa simanzi kubwa.

Wapo walioutumia kusomesha watoto elimu ya juu, wapo waliojenga ofisi ya kijiji, wapo waliojenga madarasa, maji, madaraja huku wengine wakibadili kabisa maisha yao nakuhamia mjini baada ya kupata kipato cha uhakika kupitia mradi huu.

Haya yanadhihiridhwa na Jestina Ndaisaba Bakari maarufu kama Mama Sule (Suleiman) mmoja kati ya wajasiriamali aliokuwa wakifuga vipepeo kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi na kujipatia fedha kila mwezi nakwamba wako tayari kuacha kila kitu iwapo Serikali itatangaza kuurejesha tena.

Kwa unyonge, Jestina anasema kuwa mradi huo ndiyo ulikuwa kila kitu kwake na kwa wananchi wengine na ndiyo sababu walifanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba haupotei, hata hivyo haikusaidia kitu.

“…aah jamani tupo tu, mmetunyang’anya mradi wetu wa vipepeo ulikuwa unatuingizia hela hadi Sh 600,000 tunasomesha na kuendesha familia, ila ndiyo hivyo tena bwana,” anasema Jestina.

Jestina anasema baada ya kuwa wamepata maarifa kuhusu mradi huo walijiandaa vema na kufanya kila linalohitajika kwa usahihi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaendelea kuijenga jamii yao ikiwemo kusomesha watoto kupitia fedha walizopata.

“Asikwambie mtu… tulijipanga sana tukaweka mazingira na ikafikia hatua hadi tukajua kuwa kipepeo huyu anakula majani kiasi gani na anakula mti gani.

“Nilikuwa ni mfugaji wa vipepeo hapa kijijini, tangu wamestisha mradi huu tumeathirika sana kwani ulikuwa unatusaidia kusomesha watoto.

“Pia, tulipata chumba kimoja cha darasa ambacho wanafunzi wanasomea, kwa hiyo baba kwa mwezi mtu alikuwa anaingiza Sh 200,000 hadi 600,000 kutegemea na ubora wa vipepeo wako, lakini sasahivi maisha ni magumu sana kule shambani iriki bado hadi Septemba,” anasema Jestina ambaye kwa mwonekano ni kama umri umekwenda lakini bado anapambana na maisha kwa ajili ya kusaidia familia yake kwani ndiye Mama na ndiye Baba baada ya mumewe kufariki dunia miaka michache iliyopita.

Jestina Ndaisaba Bakari, aliyekuwa akifanya biashara ya vipepeo.

Mama huyu aliyevalia gauni refu lenya maua ya rangi nyeusi na njanohuku akiwa amejitanda kitaamba chekundu kichwani kwa unyonge anasema kwa sasa maisha yamekuwa magumu sana ikilinganishwa na awali wakati wa mradi.

“Sasahivi maisha nimagumu sana, unajua ulikuwa ukiwalisha wale vipepeo wakitaga mayai ukiyaweka wakitotoa basi unapata vipepeo wengi na hapo unakuwa na fedha ya kutosha, wanunuzi walikuwa wanakuja kila wiki, hivyo tulikuwa na uhakika wa kikusanya fedha kila wiki maana tulikuwa 16 kwenye kikundi chetu, tulifanya kuanzia mwaka 2013 hadi 2016,” anasema Jestina aliyevalia kipande cha kanga chenye maneno ya kiingereza yanayosomeka Strong Women(Mwanamke Imara).

Umeacha maumivu

Jestina anasema kuwa mradi huo hata ukija leo wataacha kila kitu na kuupokea kwa mikono miwili.

“Huu ni mradi ambao hata ukija kesho tunaupokea kwa mikono miwili kwani vipepeo ukishawapa chakula unaenda zako shamba kuendelea na mambo yako, tuliwahi kuwambia wakubwa wetu watusaidie kutusemea, lakini hatukufanikiwa.

“…tuliumia sana, tukawaachia tu vipepeo wetu wakaruka na kwenda zao. Tukasema hatuna cha kufanya… na wakati huo ndiyo vipepeo walikuwa wameongezeka kuliko wakati mwingine wowote ule,”.

Jestina Bakari.

“…tuliumia sana, tukawaachia tu vipepeo wetu wakaruka na kwenda zao. Tukasema hatuna cha kufanya… na wakati huo ndiyo vipepeo walikuwa wameongezeka kuliko wakati mwingine wowote ule.

“Kwakweli mradi wetu ule unapaswa kuendelea kwani watoto wetu walisoma kwa uhakika na raha wakati ule wa vipepeo lakini sasahivi mfano nina mwingine yuko kidato cha tano huko Morogoro isivyobahati mume wangu Mwenyezi Mungu alimchukua na ndiye alikuwa ananisaidia kunikamatia vipepeo, namsomesha kwa maumivu makali sana yule mwanangu,” anasema Jestina na kuongeza kuwa:

“Mradi ule ulitupa jeuri sababu hata ukikopa dukani unga ulikuwa na uhakika kwamba mwisho wa wiki au mwezi unapata fedha, tulikuwa tunamuuzia Amiri anakuja na pikipiki yake akiwa na rafiki yake wanafika na kuchuku yale mapupa na kuondoka, kwa kweli tulifurahi sana,” anasema.

Kipepeo Picha na britannica.com

Maisha nje ya vipepeo yanahitaji uvumilivu

“Nina watoto sita kwasasa nimejikita kwenye kilimo cha iriki, karafuu na mdarasini lakini faida yake inachelewa ikilinganishwa na vipepeo kwani walikuwa wakifyonza chakula wakishiba wanatotoa mayai yakutosha, kwakweli tulianza kuwa wataalamu kwani walikuwa na uhakika wa kumwaga mayai 500 mpaka 1,000 ambapo hapo pupa moja bei ilikuwa Sh 400 hadi 3,000 kutegemea na ubora.

“Sasahivi biashara ni ngumu sana hata ukisema upike chapati bado huwezi kupata mafanikio kama kwenye vipepeo, turudishieni mradi wetu jamani haki ya Mungu tena, kwani niliweza mpaka kununua kiwanja kupitia mradi huu,” anasema Jestina.

Wasimamizi wa mradi

Amiri Shegembe ni Afisa wa Shirika la Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFCG) ambapo anakiri kuwa wananchi hao sasa wanaishi maisha duni kufuatia kupigwa marufuku kusafirisha vipepeo nje ya nchi.

Afisa wa Shirika la Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFCG), Amiri Shegembe, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mradi huo wilayani Muheza hivi karibuni.

Sheghemba anasema Mradi wa Amani Butterfly ulianzishwa katika mwaka 2004 na malengo makubwa ilikuwa kwanza kukwamua jamii ambazo zinaishi kandokando ya Misitu ya Hifadhi ya amani.

“Lengo la pili ilikuwa ni kuwakwamua akina mama kwani katika mradi huu asilimia 50 walikuwa ni wanawake na lengo la tatu lilikuwa ni kwa ajili ya mfano kwani ulikuwa ni mradi wa kwanza kabisa kunzishwa Tanzania na tulipanga kwamba iwapo ungefanikiwa basi tungesambaza elimu hii ya ufugaji wa vipepeo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” anasema Sheghembe.

Kwanini Vipepeo?

Sheghembe anasema kuwa kupitia TFCG walianzisha mradi huu wa ufugaji wa vipepeo kutokana na kuwa na soko kubwa katika mabara ya Ulaya na Amerika.

“Vipepeo wana soko kubwa Ulaya na Marekani kwani kule wanatumiwa kwa ajili ya nyumba za vipepeo ambapo watalii huingia ndani ya majumba hayo na kuangalia kwa kulipa fedha.

“Hivyo, madhumuni makubwa yalikuwa ni kuwezesha jamii zaidi kujihusisha na ufugaji wa vipepeo kama sehemu ya kujiingizia kipato kwani hatua hiyo ilikuwa ikichagiza ustawi wa maisha ya binadamu na utunzaji wa mazingira hususan misitu,” anasema Sheghembe.

Mgawanyo wa mapato

Anasema mgawanyo wa vipato wakati mradi huo ukindelea ilikuwa ni asilimia 65 ya mapato yalikuwa yakirudi kwa wafugaji wa vipepeo ambayo hiyo ilikuwa kama bei ya vipepeo.

“Ikumbukwe kuwa kipepeo mmoja wa bei ya chini tulikuwa tunamnunua kwa mfugaji kwa Sh 400 na wa bei ya juu Sh 4,000. Asilimia 28 ilikuwa inarudi kwa ajili ya kuendeshea mradi kwani ulikuwa unajitegemea wenyewe hii ikihusisha malipo ya wafanyakazi wa mradi, usafirishaji na mambo mengine.

“Asilimia 7 ilikuwa inarudi kwa ajili ya maendeleo ya jamii na hii ni fedha ambayo ilikuwa inategemea na mauzo ya kijiji kwani kama kilikuwa na mauzo makubwa basi fedha nayo ilikuwa inakuwa kubwa.

“Vijiji kupitia wananchi wao walikuwa wanaamua wenyewe kwamba hiyo fedha watumie katika nini, kuna baadhi ya vijiji kama Kisiwani ambacho kinatakribani watu 1,500 klitumia hiyo fedha kutengeneza mradi mkubwa wa maji ambapo mpaka sas hivi ndiyo maji wanayoyatumia.

“Kuna baadhi ya vijiji vingine kama Kwezitu, Msasa IBC walitumia fedha hiyo katika kuongeza madarasa katika shule za msingi na kuna baadhi ya vijiji vingine vilichagua kujenga madaraja ambayo yalikuwa yakiunganisha kijji kimoja na kingine,” anasema Sheghembe.

Afisa wa Shirika la Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFCG), Amiri Shegembe, akionyesha moja ya sehemu ambayo ilikuwa ikitumika kuhifadhia vipepeo.

Anasema pamoja na mambo mengine mafanikio mengine makubwa yalikuwa ni kusaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

“Unajua ufugaji wa vipepeo kwanza unategemea uwepo wa misitu kwa hiyo mtu anapokuwa anafanya ufugaji anaona umuhimu wa kuhifadhi misitu. Pia ilichangia ongezeko la fedha za kigeni kwani tulikuwa tunalipa wakulima kwa dola kila mwisho wa mwezi,” anasema Sheghembe.

Kukua kwa Mradi

Anasema mradi ulianza tangu mwaka 2004 ambapo tulianza kwa mauzo ya chini ya Sh milioni 20 kwa mwaka lakini kadri miaka ilivyokuwa inakwenda ndivyo ulikuwa ukiongeza thamani hadi kufikia Sh milioni 120 kwa mwaka mmoja.

“Tuliendelea hadi Machi 17, 2016 ambapo Serikali ilitangaza kustisha biashara nzima ya usafirishaji wa viumbe hai nje ya nchi na vipepeo waliangukia katika kundi hilo. Tulikuwa tunasafirisha kwenda kwenye nchi mbalimbali za bara la Ulaya na Marekani,” anasema Sheghembe ambaye anakiri kuwa mradi huo ulisaidia kuhifadhi vipepeo pamoja na wanyama wengine wanaopatikana katika Milima ya Usambara Mashariki.

Ulipendwa na kila mtu

Alphonce Nyululu ni Kaimu Mhifadhi katika Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani Nilo yenye ukubwa wa Hekta 8,380 iliyoanzishwa mwaka 1997 kwa lengo la kulinda na kuhifadhi viumbe vyote vilivyoko katika hifadhi hiyo inayozungukwa na vijiji 20.

Alphonce Nyululu ni Kaimu Mhifadhi katika Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani Nilo.

Akizungumzia mradi huo wa vipepeo anakiri kuwa ulikuwa unawapa faida sana wananchi kabla haujastishwa na Serikali.

“Wakulima wa vipepeo ni kweli wameathirika, ninachoweza kusema ni kwamba nadhani Serikali bado iko kwenye mchakato kuona ni namna gani itaendeleza mradi huu, ila ulisaidia sana wananchi kuendesha maisha.

“Tunaamini kwamba huko mbeleni utaratibu utaweza kufanyika ili kujua kwamba kipi kinatakiwa kisafirishwe na kipi kinatakiwa kubaki ili wananchi wasiweze kuathirika badala yake waweze kupata faida,” anasema Nyululu.

Serikali yawataka kuwa na subira

Hata hivyo, wakati wananchi hao wakiwa bado katika mtanziko huo juu ya lini biashara hiyo ya uuzaji wa Pupa itaendelea, Serikali imebainisha kuwa wanapaswa kuendelea kuwa wavumilivu.

Mapema Jumatatu Agosti 14, mwaka huu, Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Fortunat Msofe amenukuliwa na Gazeti la Serikali la Daily News akisema kuwa wanaendelea na jitihada za kutatua suala hilo huku akiwaomba wakulima hao kuwa na subira.

Aidha, imesisitiza kuwa inapitia faida na hasara iliyopatikana kutokana na mauzo ya wanyama pori hai kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

“Wizara inafuatilia kwa makini suala hilo, tutatoa tangazo mara tu litakapokuwa tayari,” amesema Dk. Msofe.

Hiyo ilikuwa ni sehemu ya ziara ya wanahabari wa Mazingira kuangalia ushoroba wa Amani-Nilo

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img