8.3 C
New York

Ushirikiano ni muhimu katika kudhibiti biashara haramu ya viumbe pori-Mtaalam

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na biashara haramu ya viumbe pori, bado kuna umuhimu mkubwa wa kila mtu kushiriki katika kukomesha biashara hii. Biashara haramu ya viumbe pori ni moja ya biashara haramu kubwa duniani, ikishika nafasi ya nne baada ya biashara ya dawa za kulevya, bidhaa bandia na usafirishaji wa binadamu.

Mkuu wa Kitengo cha Sera wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza, akizungumza wakati wa mdahalo huo.

Matharani katika mwaka 2023 pekee thamani biashara haramu ya viumbe na mimea pori duniani ilifikia Dola za Marekani Bilioni 23 ikilinganishwa na kiasi cha dola milioni 600 kati ya mwaka 2016 na 2018 sawa na ongezeko la mara 23 zaidi.

Mkuu wa Kitengo cha Sera wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza, alieleza kuwa biashara haramu ya viumbe pori ina athari kubwa katika nyanja za kiuchumi, kijamii, na kimazingira. Amesema biashara hiyo hufanyika kwa siri na inaendeshwa na watu wenye nguvu kubwa kifedha, hivyo inahitaji juhudi za pamoja kukabiliana nayo.

Mgaza aliyasema haya Juni 19, 2024, kwenye mdahalo maalum ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa USAID kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. Mdahalo huo, ulioshirikisha waandishi wa habari za mazingira, ulioneshwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia chaneli yake ya Safari.

Katika mdahalo huo, Mgaza alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na biashara haramu ya viumbe pori. “Biashara haramu ya viumbe pori ni tatizo kubwa, na ili kukabiliana nalo, ni lazima kuwe na juhudi za pamoja kitaifa na kimataifa. Wizara na taasisi za serikali, sekta binafsi na hata mtu mmoja mmoja, wote wanapaswa kushiriki katika kupambana na biashara hii haramu,” amesema Mgaza.

Aliendelea kusema kuwa bila ushirikiano wa pamoja, haitakuwa rahisi kupambana na biashara hiyo na uhalifu utaendelea. Juhudi za serikali na wadau mbalimbali zimesifiwa kwa hatua wanazozichukua, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kuzuia athari zinazotokana na biashara hii haramu.

Mdahalo huo umeonesha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wote na kuendeleza juhudi za pamoja katika kukabiliana na biashara haramu ya viumbe pori, ambayo inazidi kutishia ustawi wa kiuchumi, kijamii na kimazingira nchini Tanzania.

Akizungumzia mdahalo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, alisema kuwa lengo la chama hicho ni kuhakikisha kuwa kinawawezesha waandishi wa habari, hususan wa mazingira, kwa mbinu na maarifa ya kuripoti habari zinazohusiana na biashara haramu ya viumbe pori.

“JET itaendelea kuwaunganisha waandishi wa habari na wataalamu mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wanapata maarifa namna ya kuripoti taarifa za biashara haramu ya viumbe pori ili umma wa Watanzania uweze kufahamu athari za biashara hiyo haramu ikiwamo hasara ambazo taifa linapata kupitia kuendelea kuwapo kwa biashara hiyo,” alisema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img