Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MKOA wa Dar es Salaam umetajwa kuwa unaongoza kwa kukamatwa dawa za kulevya na kwamba maeneo makubwa ya starehe (klabu) na fukwe hutumika kuuza biskuti za bangi.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema serikali imejipanga kutupia jicho la ziada kudhibiti matumizi na biashara ya dawa hizo.
Akitoa taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa Mwaka 2023, Waziri Mhagama amesema idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini ni vijana kwa wastani wa asilimia 78, hali inayoathiri nguvu kazi ya Taifa.
“Mkoa unaoongoza hadi sasa ni Dar es Salaam. Tutazunguka lakini ukirudi Dar es Salaam unakutana nao. Tunashukuru sana Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imejipanga vizuri na imefanya kazi nzuri sana. Tutazunguka nchi nzima lakini kwa Dar es Salaam tumeweka kituo.
“Hadi kufikia Desemba 2023, waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipatiwa huduma katika hospitali hizo. Hii ni hatua muhimu katika kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya kama vile, uraibu, UKIMWI, kifua kikuu, homa ya ini, magonjwa ya akili na yasiyoambukiza,” amesema.
Kwa kipindi hicho, amesema mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, ilikamata kilogramu 1,965,340.52 zikihusisha watuhumiwa 10,522 (wanaume 9,701 na wanawake 821).
“Dawa zilizokamatwa ni heroin kilogramu 1,314.28, cocaine kilogramu 3.04, methamphetamine kilogramu 2,410.82, bangi kilogramu 1,758,453.58, mirungi kilogramu 202,737.51, skanka kilogramu 423.54 na dawa tiba zenye asili ya kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672,” amesema.
Pia amesema dawa hizo zilizokamatwa ni karibu mara tatu ya kiasi kilichokamatwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ambacho ni kilogramu 660,465.4.
Mhagama amesema dawa ngeni zilizoanza kuingizwa nchini hivi karibuni kama vile methamphetamine, skanka na biskuti zilizochanganywa na bangi pia zilikamatwa katika kipindi hicho.
Katika kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya, amesema serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 inayolenga mambo mbalimbali ikiwamo kuimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi.
“Sera inatoa maelekezo ya kufanya utafiti wa mazao mabadala katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha mazao hayo ili wananchi wa maeneo husika wajihusishe na kilimo cha mazao halali badala ya kilimo cha bangi na mirungi,” amesema.
Pia amesema sera inaelekeza kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya ili ushiriki wao ulete tija katika mapambano hayo
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema zaidi ya kesi 7,000 zimetolewa hukumu na serikali imeshinda kwa asilimia 83 ya kesi zote na asilimia 17 ambazo ilishindwa kwa kukosa ushahidi.
Kuhusu biskuti za bangi, Kamishna wa Kinga na Tiba wa DCEA, Dk. Peter Mfisi, amesema bei yake ni kubwa kuliko iliyotengenezwa na unga na zinauzwa kwenye klabu kubwa na fukwe.
“Mtu akinunua si kwamba amenunua kwa bahati mbaya wanataka kuwafundisha na watoto wetu ambao wazazi wana uwezo wa kuwapa Sh.1,000 kwenda nao shuleni ndio wanaolengwa sana. Wale ambao hawazijui wanapewa kama kuwafundisha ili watumie,” amesema.
Amesema biskuti hizo zilizotengenezwa kwa bangi hazina lebo na hazina shepu nzuri kama zingine na wanaonunua wanajua.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii unapokuta biskuti lazima usome, zimetengenezwa wapi, vitu vilivyotumika ukiona mtu amekuletea au hazina shepu utaingizwa kwenye utumiaji huo, ili ukizoea uendelee kutumia kila siku,” amesema.