1.4 C
New York

Watumishi mahakama watakiwa kuisoma ripoti haki jinai kuboresha uhifadhi wa wanyamapori

Published:

Na Nora Damian, Gazetini

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewaelekeza watumishi wa mahakama kuisoma ripoti ya Tume ya Haki Jinai ili kuimarisha ulinzi wa wanyamapori nchini.

Tume hiyo iliyoundwa Januari 2023 iliwasilisha ripoti yake Julai 15,2023 yenye mapendekezo mbalimbali 333.

Akizungumza leo Juni 19,2024 wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa haki jinai amesema kuna mambo mengi ambayo yametajwa katika ripoti hiyo yanayogusa shughuli za kila siku za mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, akizungumza wakati wa kikao kazi cha wadau wa haki jinai kujadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu, Dar es Salaam.

Kikao hicho kinachojadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu kimeandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ushirikiano wa Taasisi inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori (PAMS Foundation).

“Huu ni wakati wa sisi kuwa sehemu ya utekelezaji wa yale ambayo yametajwa katika tume hii. Tuwahimize watumishi na kuwasimamia wasome taarifa ya tume hii, isibaki kwa viongozi, ishuke kwa wananchi itusaidie kuboresha haki jinai, ulinzi wa wanyamapori na haki za wanyama,” amesema Profesa Juma.

Aidha amesema mafunzo hayo yamesaidia kutekeleza sheria mbalimbali katika kulinda wanyamapori na misitu na haki za binadamu.

“Maamuzi yameboreshwa zaidi baada ya kupata mafunzo kutokana na uelewa unaoheshimu uwepo wa utajiri mkubwa wa wanyamapori na misitu,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Fortunata Msofe, amesema wanatarajia mafunzo hayo yataboresha uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili na uhifadhi wa wanyamapori na kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji Profesa Paul Kihwelu, amesema mafunzo wanayotoa yanalenga kutatua changamoto za sasa na baadaye.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji Profesa Paul Kihwelu, akizungumza wakati wa kikao kazi cha wadau wa haki jinai kujadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu, Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kati ya mwaka 2022 na 2024 yalijumuisha washiriki 827 kutoka mikoa 26 na kufanyika katika vituo vya Morogoro, Katavi, Iringa, Tanga na Mara.

Washiriki ambao ni majaji wa mahakama kuu, mahakimu, waendesha mashitaka na wapelelezi wa ngazi mbalimbali wamejengewa uwezo kuboresha upokeaji wa taarifa za uhalifu wa makosa ya wanyamapori, ukamataji, upekuzi, uchukuaji na uhifadhi wa vielelezo, upelelezi, uendeshaji wa mashauri, usikilizaji, uandishi wa hukumu na utoaji adhabu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img