1.4 C
New York

Mradi wa USAID na MJUMITA ulivyobadili mtazamo wa Uhifadhi mkoani Morogoro

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Kwa miaka ya nyuma wananchi walikuwa hawaoni umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na miongoni mwa sababu za wao kufanya hivyo ilikuwa ni wengi wao kutokujiona kama wadau wa moja kwa moja wa rasilimali za misitu na wanyamapori. Walihisi kwamba hifadhi za mazingira ni mali ya serikali au taasisi za nje na hivyo hawakuhisi kuwa na jukumu la moja kwa moja katika kulinda rasilimali hizo.

Dhana hiyo iliwachochea wananchi kukosa motisha ya kushiriki katika juhudi za uhifadhi, wapo waliodhani kwamba uhifadhi unamaanisha kuzuia wananchi kutumia rasilimali ambazo walitegemea kwa maisha yao ya kila siku. Hii iliwafanya wahisi kuwa uhifadhi ni kikwazo kwa ustawi wao badala ya kuwa fursa.

Hata hivyo, kwa sehemu kubwa hii ilichangiwa na wao kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na jinsi gani uhifadhi unavyoweza kuleta manufaa ya muda mrefu kwa jamii nzima, ikiwa ni pamoja na kizazi kijacho.

Pia, miradi mingi ya uhifadhi hapo awali haikuhusisha wananchi katika hatua za awali za upangaji na utekelezaji. Kutokuhusishwa huko kulisababisha hisia za kutengwa na kutojihusisha na miradi hiyo.

Umaskini na matatizo ya kiuchumi pia yalichangia kutokujali uhifadhi wa mazingira. Wananchi walikuwa na wasiwasi zaidi kuhusu mahitaji yao ya kimsingi kama chakula, makazi, na afya, na hivyo hawakutoa kipaumbele kwa masuala ya uhifadhi.

Kukosekana kwa ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka za uhifadhi kulisababisha migogoro na vitendo vya ujangili. Baadhi ya wananchi waliona kwamba wanapaswa kuchukua hatua za kinyume cha sheria ili kujipatia kipato kupitia rasilimali za misitu na wanyamapori.

Afisa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili-MJUMITA, Kelvin Shirima, akizungumza na Waandishi wa Habari za Mazingira, hawapo pichani.

Kwa kuzingatia changamoto hizi, miradi kama ya USAID Tuhifadhi Maliasili imejitahidi kubadilisha mtazamo huu kwa kuwaelimisha wananchi, kuwaonyesha faida za moja kwa moja za uhifadhi, na kuwahusisha moja kwa moja katika miradi ya uhifadhi. Hii imeongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika kulinda mazingira yao.

Ni wazi kuwa uwepo wa wadau wa maendeleo kama Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na taasisi za ndani umefanikisha kupunguza kabisa dhana kwamba wananchi hawahusiki na ulinzi wa maliasili za misitu. Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) na taasisi nyingine ikiwemo Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), umefanikisha kufanya uhifadhi kuwa agenda ya kudumu kwenye vijiji vilivyopo wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.

Kelvin Shirima ni Afisa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili-MJUMITA, ambapo nasema kuwa wamefanikisha suala la uhifadhi kuwa agenda ya kudumu kwenye mikutano ya vijiji, tofauti na ilivyokuwa awali. Shirima anasema kuwa MJUMITA imekuwa ikifanya kazi na vikundi vinavyojihusisha na masuala ya mazingira kwenye mitandao 129 iliyopo katika kanda sita, mikoa 14, wilaya 32, na vijiji zaidi ya 452.

“Tumekuwa tukishirikiana na vikundi kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya misitu. Lengo letu ni kuhakikisha jamii inajua umuhimu na thamani ya kulinda na kunufaika na maliasili zilizopo kwenye maeneo yao, hasa misitu na wanyamapori,” anasema Shirima.

Shirima aliongeza kuwa MJUMITA pia inaliangalia suala la utawala bora kwenye ngazi za vijiji wanavyofanya kazi navyo na kuangalia utekelezaji wa mradi wa urejeshaji wa shoroba ya Nyerere Selous-Udzungwa kwa kushirikiana na taasisi za mazingira zilizopo wilayani Kilombero.

“Tunafanya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali kwenye jamii kwa kutumia mfumo wa Pima Kadi, hasa katika vijiji vya Sole, Mang’ula A, na Kanyenja. Utendaji wetu unajumuisha jamii kwa kukusanya makundi mbalimbali ya kijamii na kuwapa jukumu la kuangalia uwajibikaji wa viongozi kwa kutumia mfumo unaojulikana kama Social Accountability Monitoring (SAM),” alisema Shirima.

MJUMITA imefanikiwa kutoa mafunzo ya ufuatiliaji huo kwa zaidi ya watu 50 wa vijiji vya Mang’ula A na Msolise. “Hawa tunaowapa mafunzo ya ufuatiliaji, na wao wanafuatiliwa kwa kuwapa fomu ambazo zina alama za ubora, kuanzia alama moja mpaka tano. Mfuatiliaji akipata alama za chini mara kwa mara anakosa sifa ya kuendelea na kazi hiyo,” anasisitiza Shirima.

Benedict Minja kutoka MJUMITA.

Benedict Minja kutoka MJUMITA alisema moja ya mambo yanayowafurahisha ni kuona vijiji vinaipa thamani agenda ya uhifadhi, jambo ambalo linaongeza kasi na ubora wa kulinda hifadhi. Salum Mnanga, mkazi wa Kijiji cha Mang’ula A, alisema elimu inayotolewa mara kwa mara na MJUMITA imewasaidia kufaidika na rasilimali za misitu na kwamba sasa wanavijiji wengi wanashiriki katika ulinzi na utunzaji wa rasilimali hizo.

Sehemu ya waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo (kushoto) na Mwandishi wa Habari wa Gazeti la The Guardian, Felister Peter, wakifuatilia wasilisho kutoka kwa wawakilishi wa MJUMITA(hawapo pichani).

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo, aliipongeza MJUMITA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye ulinzi wa maliasili za misitu kwa kushirikisha jamii zilizopo pembezoni mwa hifadhi. Kwa juhudi hizi, wananchi sasa wanahisi kuwa sehemu ya uhifadhi na wanajitahidi kulinda maliasili kwa manufaa ya wote.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img