21 C
New York

Visual| Shoroba 7 Tanzania zitakazomulikwa na mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini, Tanzania ina jumla ya shoroba 61 ambapo 41 zipo hatarini kutoweka kutokana na kuvamiwa na shughuli za kibinadamu huku shoroba 20 kati ya hizo zikiwa zimezibwa kabisa.

Miongoni mwa athari za binadamu kuvamia shoroba hizo ni pamoja na kuwepo kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyama ambapo mara nyingi wanyama huripotiwa kusababisha uharibifu wa mali au vifo kwa wanyama na binadamu.

Katika kulikabili hilo, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET) chini ya Ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani(USAID) kupitia Mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili inalenga kuangazia hatari ya ya kutoweka kwa wanyamapori na viumbe hai nchini kwa kuangalia hali ya shoroba saba.

Akizungumza na Gazetini Mjini Bagamoyo mkoani Pwani, Mkurugenzi wa JET, John Chikomo amesema Mradi wa Tuhifadhi Maliasili ni wa miaka mitano na unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyama na viumbe hai nchini Tanzania.

“Mradi wa tuhifadhi Maliasili unahusisha shoroba ya wanyamapori uliopo Kwakuchinja ambao unaunganisha mfumo wa Ikolojia wa Tarangire-Manyara katika Wilaya za Babati na Monduli zilizopo kwenye Mikoa ya Manyara na Arusha.

“Pia kuna Shoroba ya Kigosi Moyowosi-Burigi Chato-unaounganisha Kigosi Moyowosi na Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato zilizopo katika Wilaya za Biharamulo na Kakonko, Mkoa wa Kagera na Kigoma,” anasema Chikomo na kuongeza kuwa:

“Kuna shoroba ya  Nyerere Selous-Udzungwa- unaounganisha Hifadhi za Taifa za Milima ya Nyerere Selous na Udzungwa, katika Mji wa Ifakara, Mkoa wa Morogoro, nyingine ni shoroba ya Amani- Nilo inaounganisha Hifadhi ya Mazingira ya Amani na Hifadhi ya Misitu ya Mazingira ya Nilo, katika Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga,” amesema Chikomo.

Kwa mujibu wa Chikomo, shoroba ya Ruaha Rungwa-Katavi inaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Pori la Akiba la Rungwa, Mapori ya Akiba ya Lukwati na Pigi, na Katavi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.

“Kuna shoroba ya Ruaha Rungwa-Inyonga unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, na Mapori ya Akiba ya Rungwa na Inyonga, katika Wilaya za Itigi/Sikonge, Mkoa wa Singida/Tabora. Shoroba ya  Mahale-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale na Katavi, katika Wilaya za Tanganyika na Uvinza, Mikoa ya Katavi na Kigoma.

“Kupitia USAID mradi wa Tuhifadhi Maliasili, JET itaweka mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari kufanya uchunguzi na kuripoti ipasavyo masuala ya uhifadhi hasa kwa kuangali hali ya shoroba hizi saba ambazo tumezichagua,” amesema Chikomo.

Akizungumzia eneo hilo la shoroba, Dk. Elikana Kalumanga kutoka RTI International ambaye ni Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, anasema mradi huo unatekelewza katika shoroba hizo saba umekuwa na matokeo mazuri.

“Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kwa kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wake tayari umekuwa na mafanikio makubwa katika maeneo husika kutokana na kuwepo kwa mwamko kwa wadau wengine kuelekeza nguvu kwenye shoroba zingine,” alisema Dk. Kalumanga.

Afisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Ruben Magandi.

Upande wake Afisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Ruben Magandi amesema, TFS inashiriki kutunza na kuendeleza shoroba hasa kwa kuhamasisha katika upandaji miti.

“Sisi tunashirikiana na taasisi zingine za kisheria na za usimamizi wa maliasili zilizopo kwenye shoroba mbalimbali na tumeona mwamko ni mkubwa kwa jamii kushiriki,” aamesema Magandi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img